Kenya ina msururu ya mikataba mibovu ya kifedha, yote ikila kwa mlipa ushuru – Taifa Leo


KATIKA matukio machache mno ambayo niliwahi kutaniana na aliyekuwa mhariri msimamizi wangu enzi nikiandikia gazeti hili kama ripota, bwana mkubwa huyo alinishinikiza kutotumia akili kama kofia.

Mhariri huyo (jina lake nimelibana) akiniambia ninazo tele kichwani, ila sharti zifanyishwe kazi. Vinginevyo, fuvu lenye ubongo mzembe ni sawa na kopo la uji. Nitamuiga niseme kuwa Wakenya wana akili nyingi, lakini ni lazima wazifanyishe kazi, lau sivyo wajihini wenyewe.

Wiki jana nilikwazika sana nilipowaona wabunge wakishangilia kijinga pale Rais William Ruto alipowatangazia kuwa amefuta mikataba yote ambayo serikali yake iliandikiana na kampuni ya kimataifa ya Adani Group.

Kwanza nilijiliwaza kwamba tatizo ni wabunge wetu, ambao kwa hakika wananchi wamepoteza imani nao, ila nikaishia kutamauka pale baadhi ya wananchi walipokimbia mtandaoni kusifia uamuzi huo.

Nilizugika akili nikajiuliza Kenya imekuwa nchi ya aina gani! Hivi Wakenya ni mazuzu wasiofikiri, wajanja wa kujipa hamnazo, au watu waovu ambao mshipa hauwapigi hata mambo yakienda tenge?

Tuambizane ukweli: Huo si uamuzi wa kupongezwa kabla ya mtu kutafakari kuhusu chanzo na athari zake. Chanzo cha uamuzi huo wa Dkt Ruto ni kwamba mmiliki wa kampuni hiyo, Bw Gautam Adani, alifunguliwa mashtaka ya ufisadi na serikali ya Amerika.

Jiulize maswali haya: Adani asingefunguliwa mashtaka na taifa hilo tajiri zaidi duniani, Rais Ruto angefuta mikataba hiyo? Kwa nini rais hakuchukua hatua hiyo tangu zilipozagaa habari kwamba Bw Adani ni fisadi wa kutupwa aliyezama kwenye kashfa kadha nchini India alikozaliwa?

Ilikuwa lazima Waamerika wamshtaki bwanyenye huyo ndipo rais wa taifa dogo la Afrika achukue hatua kuinusuru nchi yake? Hivi Dkt Ruto anaitumikia Kenya au Amerika? Ni kitu gani ambacho kingemtendekea Dkt Ruto asingeifuta mikataba hiyo?

Ukiwa katika shughuli hiyo-hiyo ya kujiuliza maswali, tafadhali usisahau kujiuliza iwapo pesa za Wakenya zilipotelea kwenye ufutaji huo wa mkataba. Usichoshe akili zako, jawabu ya swali hilo ninayo.

Kikawaida, kote duniani, mkataba unapofutwa, anayeufuta humlipa mbia mwenzake fidia fulani. Hivyo ndivyo sheria za mikataba zinavyofanya kazi, wala haijalishi mikataba inafutwa kwa sababu gani.

Mradi tu watu walitia saini mkataba kwamba wangefanya shughuli fulani pamoja, anayejiondoa kwenye mkataba huo anapata hasara. Viongozi wetu wangakanusha kiasi gani, Kenya haiwezi kuepuka hasara katika kisa cha Adani.

Mkenya anakabiliwa na tatizo kubwa zaidi kwa kuwa anayepaswa kumtetea ili asigharamike zaidi huwa na nia ya kulipa hasara za aina hiyo haraka iwezekanavyo kwa kuwa anafadika kwa njia moja au nyingine.

Unapotafakari kuhusu hilo, tilia maanani habari kwamba inadaiwa Adani alilipa hongo ya Sh9 bilioni na ushei ili kupewa mikataba hiyo ya thamani ya zaidi ya Sh950 bilioni. Inaitwa ahsante ya asilimia 1 eti.

Ukizingatia kwamba Adani hawezi kukubali kupoteza Sh9 bilioni alizotoa, uongeze na ada ya kuvunjiwa mikataba, kisha ukumbuke kuwa hasara yote hiyo italipwa nawe nami, kichwa kisipokuwanga una tatizo!

Yaani kazi yao kula tu, hata kwa mikataba mibaya inayoingiwa makusudi, nasi yetu kulipa hasara! Mbona hakuna uwiano kati ya haki na matendo ya mtu katika ulimwengu wa mafisadi?

Ukiangalia historia ya Kenya vizuri, hasa ukichunguza serikali hii na nyingine nne zilizoitangulia, utapata kwamba imekuwa kawaida kwa viongozi wetu kuingia mikataba mibaya, nasi wananchi huishia kulipa hasara kubwa.

Jomo Kenyatta, japo hili huambiwi sana, hakuwajibikia hela ambazo serikali yake ilikopeshwa na Uingereza ili ilinunue mashamba yaliyokaliwa na walowezi wa Uingereza walioishi Kenya kabla ya taifa letu kuwa huru.

Kipawa cha mzee huyo cha kukosa aibu katika unyakuzi wa ardhi kinanisadikisha kuwa Kenya haina watu wabunifu na jasiri kamili kwa maana hakijaandikiwa hadithi za kubuni na za kitawasifu.

Mkabata muovu wa Goldenberg ambao marehemu Daniel Moi na serikali yake ya Kanu waliingia na bwanyewe Kamlesh Pattni uliishia kwa Wakenya kugharamika pakubwa.

Rais Mwai Kibaki alipoingia madarakani tu nusra asombwe na dhoruba ya sakata za Anglo-Leasing, na aliposhinikizwa sana kuzihusu akadai kuwa ilibidi alipie huduma nyingi tu ambazo Kenya haikupata, kisa na maana mikataba hiyo ilikwisha kutiwa saini na serikali ya Moi!

Kisingizio kama hicho kilitolewa na serikali ya sasa mara tu ilipoingia madarakani, ikasema eti ililazimika kufidia kampuni za mafuta na unga ambao zilikuwa zimeingia mikataba ya kupunguza bei na serikali ya Uhuru Kenyatta.

Natumai hujasahau kwamba serikali ya Uhuru ilijipaka tope kwa sakata ya mabwawa ya Arror na Kimwarer, ambayo Dkt Ruto, wakati huo naibu rais, alipuuzilia mbali kama sakata ndogo iliyowagharimu Wakenya Sh7 bilioni pekee. Nipe Sh7 bilioni uone kazi zinayoweza kufanya.

Kwa kuwa inaonekana nchini Kenya ni sharti kila serikali iwe na kashfa yake, na hii ya sasa tayari imejichafulia jina kwa mikataba ya Adani chini ya miaka mitatu tangu iliposhika hatamu za uongozi, hudhani kwamba itatuacha katika hali mahututi?

Kama mwandishi natamani kukupa matumaini, lakini pia naogopa kutenda dhambi ya kukudanganya kwa kuwa ukiujua ukweli utaniona mnafiki.

Badala ya kukupaka mafuta kwa mgongo wa chupa, nakupa changamoto: Kataa vishawishi vya kuwa mwizi au fisadi, mabadiliko ambayo unatamani kuona nchini Kenya yanakutegemea wewe binafsi.

[email protected]



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*