Kenya yachoma picha raia wa kigeni 50 wakitekwa – Taifa Leo


KWA miaka mingi, raia wa kigeni walidhani Kenya ni mahali salama ambapo wangekimbilia kupata hifadhi baada ya kudhulumiwa nchini mwao. Lakini hali haijakuwa hivyo.

Ndani ya miaka minne iliyopita, angalau raia 50 wa kigeni wamekamatwa au kutekwa nyara nchini Kenya kwa njia ya kutatanisha.Kwa mfano, mnamo Jumatatu wiki hii, mwanahabari Mtanzania Maria Sarungi alidai kutekwa nyara Jumanne na wanaume wanne kutokana na shinikizo kutoka taifa lake.

Bi Sarungi aliyeonekana kuchanganyikiwa, alisema aliachiliwa huru baada ya kuzungushwa na kuhojiwa kwa saa kadhaa.Hakutambua eneo ambako aliachiliwa.

Kutekwa nyara kwa Bi Sarungi kulijiri miezi miwili baada ya mwanasiasa wa Uganda, Kizza Besigye kutekwa nyara jijini Nairobi na kusafirishwa hadi nchini mwake kufunguliwa mashtaka katika mahakama ya kijeshi.

Besigye, ambaye ni hasidi wa miaka mingi wa Rais Museveni, alishtakiwa kwa kosa la kumiliki bunduki kinyume cha sheria akiwa Kenya.

Haieleweki ni kwa nini alishtakiwa katika mahakama ya kijeshi nchini Uganda kwa kosa alilodaiwa kutenda akiwa Kenya.

Besigye alikamatwa nchini Kenya ilhali Rais Museveni mwenyewe na mkewe Janet, wamewahi kupewa hifadhi nchini baada ya kuhepa udhalimu kutoka kwa aliyekuwa kiongozi wa Uganda, dikteta Idi Amin katika miaka ya 1970.

Nyakati hizo, Kenya ilikuwa salama kwa raia wa kigeni bila kujali tofauti kati yao na serikali zao.

Lakini hali ni tofauti wakati huu kwani kabla ya kutekwa nyara kwa Sarungi na Besigye, raia wa Uturuki pia walitekwa nyara.Watu hao; Mustafa Genç, Abdullah Genç, Hüseyin Yesilsu, Necdet Seyitoglu, Oztürk Uzun, Alparslan Tascı na Saadet Tascı walitekwa nyara Oktoba mwaka jana.

Mbw Genç, Yesilsu, Uzun and Tascı walikuwa wakimbizi waliotoroka Uturuki na walikuwa chini ya ulinzi wa Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, walikamatwa na kurejeshwa kwa nguvu nchini mwao na wakasukumwa gerezani.

Bw Uzun alipewa kitambulisho kama mkimbizi mnamo Januari 2024 ilhali Bw Mustafa alipewa kitambuliwa mnamo Julai, 2023.Bw Tasci alipata kitambulisho cha kumtambua kama mkimbizi mnamo Oktoba 2020 huku Bw Huseyin alipata stakabadhi hiyo mnamo Januari 2021.Wamekuwa wakosoaji wa Rais Reccep Tayip Ergogan.

IMETAFSIRIWA NA CHARLES WASONGA



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*