Kenya yahisi joto Trump kutua Ikulu kufuatia hatari ya kutimua raia na kuikosesha nchi pesa – Taifa Leo


KENYA imeanza kuhisi joto kutokana na sera za Rais Donald Trump za kuondoa Amerika kutoka Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO).

Na sasa, inachunguza mikakati mbalimbali ya kuimarisha mifumo yake ya afya na kushughulikia changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na uamuzi huo.

Sera za Trump zinatarajiwa kuathiri uchumi wa Kenya baada yake kutisha kutimua wahamiaji ambao wanatuma mabilioni ya pesa nyumbani kila mwaka.

Serikali ya Kenya Kwanza imekuwa ikilenga Wakenya wanaoishi ng’ambo kuimarisha mapato yake na wengi wao wako Amerika.

Mwaka jana, Wakenya wanaoishi ng’ambo walitumia nchini zaidi ya Sh640 bilioni kwa mujibu wa takwimu za Benki Kuu ya Kenya.

Zaidi ya asilimia 50 ya pesa hizi zilitoka kwa Wakenya wanaoishi Amerika.

Kuna zaidi ya Wakenya 30,000 ambao wanaweza kuathiriwa na sera ya Trump ya kutimua raia wa kigeni wanaoishi Amerika hasa wasio na stakabadhi halali.

Bw Trump ametangaza kuwa atatoza ushuru bidhaa zote zinazoingizwa Amerika hatua ambayo itakuwa pigo kwa Kenya ambayo imekuwa ikiuza nguo nchini humo chini ya mkataba wa biashara ya masharti nafuu kati ya Afrika na Amerika maarufu kama AGOA.

Chini ya mkataba huu, Kenya imekuwa ikiuza bidhaa za mabilioni Amerika na hatua ya Trump inaweza kufanya kampuni za kutengeneza nguo zinazouzwa nchini humo kufungwa na maelfu kupoteza ajira.

Tayari serikali ya Kenya imeanza kusaka njia za kuimarisha ushirikiano na Amerika kufuatia hatua ya Trump.

Mkurugenzi Mkuu wa Afya Dkt Patrick Amoth alisema Kenya inalenga kuimarisha ushirikiano wa afya na mataifa na taasisi nyingine ili kujaza mapengo ya ufadhili na utaalamu yaliyoachwa na hatua ya Amerika.

“Ushirikiano na washirika wa kimataifa ni muhimu ili kuhakikisha vipaumbele vyetu vya afya haviathiriwi,” Dkt Amoth aliwaambia waandishi wa habari katika makao makuu ya wizara Jumatano, Januari 22.

Dkt Amoth alisisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya afya ya kikanda kwa kufanya kazi kwa karibu na nchi jirani ili kuboresha miundombinu ya afya, kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa na kuwezesha uratibu wa kukabiliana na changamoto za afya zinazojitokeza.

“Kuimarisha ushirikiano wa kikanda ni muhimu ili kukabiliana na changamoto za afya mipakani. Ni lazima tushirikiane kama kanda ili kulinda afya za watu wetu,” alisema.

Mkurugenzi mkuu pia alisisitiza haja ya kuongeza fedha za ndani kwa afya kusaidia mipango muhimu na kupunguza kutegemea fedha kutoka nje.

Mnamo Jumatatu, Amerika ilitangaza nia yake ya kujiondoa WHO, hatua ambayo inaashiria mabadiliko makubwa katika diplomasia ya afya ya kimataifa na ina athari kubwa kwa afya ya umma, haswa katika nchi kama Kenya.

Zaidi ya miongo saba, ushirikiano kati ya Amerika na WHO umetekeleza jukumu muhimu katika kupambana na tishio kwa afya duniani, kuanzia kutokomeza ndui hadi mapambano dhidi ya Ukimwi malaria na kifua kikuu.

Kwa kuwa Amerika imekuwa mfadhili mkubwa zaidi wa kifedha wa WHO, ikitoa takriban asilimia 18 ya ufadhili wake wote, kuondoka kwake kunaacha pengo la kifedhaambalo linaweza kuvuruga mipango muhimu ya afya duniani kote.

Mipango inayoungwa kama vile Mpango wa Dharura wa Rais wa Kukabiliana na Ukimwi (PEPFAR) imekuwa muhimu katika vita dhidi ya Ukimwi, kutoa tiba ya kurefusha maisha (ART) kwa mamilioni ya Wakenya.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*