SENETA wa Kaunti ya Busia, Okiya Omtatah, amesema kwamba Kenya inahitaji kiongozi mwadilifu wa kuiokoa katika utawala mbaya unaofanya uchumi kuvurugika.
Akizindua rasmi kamati ya kutathmini ufaafu wake kama mgombeaji urais Jumatano, Bw Omtatah alisema wakati umefika wa Kenya kukombolewa katika uongozi uliofaa.
“Taifa hili linahitaji kwa dharura ukombozi kutokana na uongozi mbaya. Tunataka serikali inayosikiliza na kuheshimu nguzo ya uadilifu wa mamlaka. Mimi ni mmoja kati ya watu wanaosisitiza mtindo bora wa uongozi ambapo raia wanashirikishwa katika kufanya maamuzi,” alisema.
Bw Omtatah alisema, “Serikali zinazokosa kuzingatia sheria na kushirikisha umma katika uongozi, huwa zinachochewa na udikteta, ulaghai na ufisadi.”
Bw Omtatah, aliyezaliwa 1964 katika kijji cha Kwang’amor, Kaunti ya Busia, anataka kuwa rais wa sita wa Kenya, katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Mwanasiasa huyo ambaye ni mtaalam wa Falsafa, alishinda kiti cha useneta wa Busia katika uchaguzi mkuu wa 2022 alipozoa kura 171,681 kupitia tiketi ya chama cha National Reconstruction Alliance (NRA) na kumbwaga Hillary Itela wa chama cha ODM aliyepata kura 59,276.
Kamati hiyo ya wanachama 10 inayoongozwa na Bi Mary Kathomi, itashirikisha wadau kukusanya maoni kuamua iwapo Bw Omtatah kushinda anaweza kushinda urais.
Bw Omtatah – ambaye amesema ndoto yake ilikuwa awe kasisi wa Kikatoliki kabla ya changamoto za kiafya kukatiza safari yake –ananuia kujiunga na kinyang’anyiro cha urais ambacho Rais William Ruto anatarajiwa kuwania muhula wa pili.
Bw Omtatah Alhamisi alieleza Taifa Leo kuwa safari ambayo ameanza ni ya kupima nguvu, udhaifu, fursa na ufaafu wa azma yake.
“Huu ni ulimwengu wa data, ni pale tu unapokuwa na maelezo thabiti yanayoungwa mkono na data unapoweza kufanya maamuzi ya busara. Hiyo ndiyo hatua ya mwanzo ya azma yangu ya urais,” alisema.
Kamati hiyo inajumuisha wataalamu wa siasa, wanaharakati, na wasomi wa sheria. Masharti ya Bw Omtatah yanajumuisha kufanya kura ya maoni kote nchini ili kukusanya data inayoweza kutumika kwenye azma yake.
Mwanaharakati huyo maarufu anafahamika kwa misururu ya kesi zake dhidi ya serikali akipinga anachoona kama maamuzi ya kutiliwa shaka ya serikali.
Aliwasilisha pia kesi ya kupinga uchaguzi wa urais 2022 baada ya Ruto kutangazwa mshindi. Uanaharakati wake umewakera watu mashuhuri kiasi cha kutishiwa na kujeruhiwa.
Hata aliwahi kujifunga minyororo kwenye ua wa makao makuu ya polisi, Vigilance House, kulalamikia alichodai kuwa ukatili dhidi ya Wakenya mnamo 2008.
Baada ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN) kusomea shahada ya digrii katika Taaluma ya Biashara, Bw Omtatah alikatiza masomo yake na kujiunga na chuo cha St Augustine, Bungoma, kusomea Falsafa.
“Niliugua baada ya kukamilisha masomo yangu ya Falsafa, niliathiriwa pakubwa na ugonjwa wa kifafa. Niliambiwa siwezi kuwa kasisi nikiwa na kifafa,” alisema 2022 katika mahojiano kwenye Citizen TV.
Bw Omtatah alifichua vilevile kwamba alitafuta matibabu na hatimaye akapona.
“Baba yangu alilipa Sh1,500 na nikaanza matibabu 1987, nilipona baada ya siku 12,” alisema.
Leave a Reply