TIMU ya voliboli ya Kenya upande wa kinadada almaarufu Malkia Strikers imepangwa katika ‘kundi la kifo’ kwenye michuano ya Kombe la Dunia la Shirikisho la Voliboli Duniani (FIVB) itakayoandaliwa nchini Thailand mwaka ujao.
Vipusa hao wamepangwa katika Kundi G huku wawakilishi wengine wa bara Afrika ambao ni Misri na Cameroon wakitiwa katika Kundi A na H mtawalia.
Kundi G linajumuisha Kenya, Poland, Ujerumani na Vietnam.
Kenya itakuwa na kibarua kigumu inapozingatiwa kuwa ni siku chache zilizopita tangu izabwe na Poland kwa seti 3-0 kwenye Michezo ya Olimpiki makala ya mwaka huu iliyoandaliwa jijini Paris, Ufaransa.
Mataifa ya Poland na Ujerumani yako juu ya Kenya katika jedwali la mchezo wa voliboli ulimwenguni.
Poland inashikilia nafasi ya sita nayo Ujerumani inakamata nafasi ya 12 kwa alama 349 na 222 mtawalia.
Kenya iinaorodheshwa katika nafasi ya 22 kwa alama 152 nayo Vietnam, taifa pekee lililo chini ya Kenya, inashikilia nafasi ya 33 kwa alama 112.
Kenya ilifuzu kwa kindumbwendumbwe hicho baada ya kuibuka mabingwa wa Kombe la Afrika (CAVB) lililoandaliwa jijini Yaounde, Cameroon mwaka uliopita.
Malkia Strikers waliokuwa chini ya kocha Luizomar de Moura na Paul Bitok waliibuka mabingwa kwa kunyamazisha Pharaohs ya Misri kwa seti 3-0.
“Ni kweli tumepangwa kundi gumu lakini itategemea na maandalizi yetu,” alisema naibu mwenyekiti wa Shirikisho la Voliboli Kenya (KVF), Bitok.
Aliongeza kuwa wanapania kuweka mikakati kabambe kuhakikisha Kenya inafanya kweli kwenye kipute hicho.
Kwenye nusu fainali za Kombe la Afrika, Malkia Strikers ilifinya Cameroon kwa seti 3-1 nayo Misri ikasajili ushindi wa seti 3-0 dhidi ya Rwanda.
Misri iko katika Kundi A ambalo pia linashirikisha Thailand, Uswidi na Uholanzi.
Nalo Kundi H linajumuisha Cameroon, Serbia, Japan na Ukraine.
Mashindano ya mwaka ujao yanayoanza Agosti 22, yatashirikisha jumla ya timu 32 ambazo zimepangwa kwa makundi manane.
Leave a Reply