Kibarua cha Kindiki kutakasa serikali – Taifa Leo


NAIBU Rais Kithure Kindiki hana wakati wa kufurahia hadhi yake mpya baada ya kula kiapo huku akitetea vikali sera, miradi na maamuzi ya serikali.

Tangu kuapishwa kwake Novemba 1, Prof Kindiki alianza moja kwa moja kutetea sera tata za serikali ambazo zimeibua shutuma kutoka kwa Wakenya.

Wakati wa kuapishwa, mkubwa wake Rais William Ruto alikiri hadharani kwamba alikuwa ‘mpweke’ katika urais, Prof Kindiki alikuwa na kazi ngumu ya kueleza sera za serikali.

Wakati wa kuapishwa kwake, Prof Kindiki alimhakikishia Rais kuwa atamuunga mkono ili kuhakikisha anapeleka nchi katika ngazi ya juu zaidi.Mwezi mzima wa Novemba umeshuhudia Prof Kindiki akizunguka maeneo mbalimbali ya nchi akielezea sera za serikali.

Kuanzia Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), kuundwa upya kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), hadi mageuzi katika sekta ya chai na kahawa na mpango wa kupata kazi nje ya nchi, Prof Kindiki amekuwa akitetea mipango hii.

Hii imefanywa kuwa mbaya zaidi na ukosoaji unaozidi, hasa kutoka kwa KanisaMbunge wa Gatanga Wakili Muriu alisema Naibu Rais amekuwa sehemu ya serikali ambapo baadhi ya maamuzi kuhusu miradi hiyo yalifanywa kwa hivyo hana chaguo ila kuchukua jukumu la pamoja.

‘Iwapo serikali itafaulu au la ni hadithi nyingine lakini angalau sasa tunaona naibu wa rais akimuunga mkono bosi wake katika kueleza sera za serikali, jambo ambalo lilikosekana wakati wa Gachagua,’ mbunge huyo alisema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Moi Masibo Lumala alisema Prof Kindiki aliingia ofisini wakati mambo yalikuwa moto kwa serikali na ukosoaji unazidi kuwa mkali.

Hata hivyo, Prof Lumala anasema Rais Ruto bado yuko imara kutetea sera za serikali huku analofanya Prof Kindiki ikiwa kumuunga mkono bosi wake.

‘ Anafaa kuzingatia jambo ambalo Wakenya wanaweza kujitambulisha nalo. Angalau Gachagua alijulikana kwa ajenda ya murima, kahawa na chai. Prof Kindiki anahitaji kuchagua kitu kama muundo mpya wa elimu na kuwahakikishia vijana kwamba hakuna mtu atakayefungiwa nje kwa sababu ya karo.” Prof Lumala alisema.

Kuhusu Mamlaka ya Afya ya Kijamii (SHA) ambayo imesababisha uchungu miongoni mwa Wakenya wengi, Prof Kindiki amekiri kuwa kuna changamoto chache zinazoikabili.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa mambo yako sawa licha ya kuwepo kwa hali ya taharuki.

‘Tumeanzisha mfumo mpya wa afya ambao utahakikisha watu ambao wana mapato ya chini wanapata huduma bora za afya sawa na matajiri,’ alisema akiwa Laisamis, Kaunti ya Marsabit.

Kuhusu mashambulio makali ambayo kanisa la limeelekeza kwa serikali, haswa kuhusu uzembe wa serikali katika kushughulikia afya, ufisadi na masala ya gharama ya maisha yanayoathiri Wakenya, Prof Kindiki pia amejitokeza kulitaka kanisa kukomesha mashambulio yasiyofaa dhidi ya utawala wa Ruto.

“Viongozi wote wana uhuru wa kuwasilisha maoni yao kuhusu jinsi ya kufanya Kenya kusonga mbele. Lakini lazima wafanye hivyo kwa upendo na uzalendo. Tusiwe watu wasio na heshima na wachochezi,” alisema.

Kuhusu uundaji upya tata wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Prof Kindiki pia amejitokeza vikali kutetea serikali kuhusu mkwamo huo akisema mkono wa serikali umefungwa na kesi mahakamani.

Akizungumza akiwa Navakholo, Kaunti ya Kakamega wikendi iliyopita, Prof Kindiki alieleza kuwa agizo la mahakama la kuzuia kubuniwa kwa jopo la kuunda IEBC linazuia serikali kusonga mbele na mchakato wa kuunda upya.

Naibu rais pia ametetea mpango wa kazi ng’ambo akisema isifafanuliwe kuwa serikali inawapeleka raia wake katika mataifa ya nje.

“Hatuwatupi watu wetu katika mataifa mengine bali tunawapatia nafasi za kazi nje ya nchi, ili kujikimu kimaisha, kutumia ujuzi wao na kuwekeza tena nyumbani,” Prof Kindiki alisema wiki hii akiwa KICC.

Akiwa Mombasa wakati wa Kongamano la Chai Kenya, Prof Kindiki alisema serikali ingali imedhamiria kuboresha sekta hiyo kupitia mageuzi ya kisera na kiutawala.

Katika kuondoa dhana ya ukabila ambao mtangulizi wake alishutumiwa kueneza, Prof Kindiki tangu ashike wadhifa huo amejaribu kuzuru sehemu mbalimbali za nchi ili kujionyesha kama kiongozi wa kitaifa.

Kufikia sasa amezuru Mwingi kaunti ya Kitui, Laisamis kaunti ya Marsabit, Ndia kaunti ya Kirinyaga, Mwatate kaunti ya Taita Taveta, Kakamega na Eldoret.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*