HUKU nyota yake kisiasa ikiendelea kudidimia Mlima Kenya, Rais William Ruto ameamua kusaka uungwaji mkono eneo la Magharibi mwa Kenya ili ashinde tena katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Kando na ziara zake za kila mara eneo hilo, Rais ameunda kundi la washirika watakaomsaidia kuvumisha ajenda yake ya maendelea, maarufu kama BETA ili kuvutia upande wake wapiga kura milioni 2.2 za jamii ya Waluhya.
Dkt Ruto pia anaonekana kulenga kutumia ukuruba wake na kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga kujinadi kwa wakazi.
Bw Odinga ana ufuasi mkubwa katika eneo hilo, haswa kaunti za Kakamega, Busia na Vihiga, ambako amekuwa akizoa kura nyingi haswa katika chaguzi za 2013, 2017 na 2022.
Wandani ambao Rais Ruto analenga kuwatumia kumpigia debe katika eneo la Magharibi linashirikisha wanasiasa wenye uzoefu mkubwa na vijana wenye nguvu wenye uwezo wa kuwakabili wakosoaji wa serikali yake.
Wanaongozwa na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula.
Ili kuonyesha kujitolea kwake kutekeleza kibarua hicho, Bw Mudavadi amekivunja chama chake cha Amani National Congress (ANC) kuungana na chama cha United Democratic Alliance (UDA) miaka miwili kabla ya uchaguzi mkuu ujao.
“Chama change cha ANC kiliamua kuungana na UDA kwa sababu huo ndio mkondo ambao nchi inaelekea,” Bw Mudavadi akaripotiwa akisema.
Juzi, wakati wa ziara ya Rais Ruto katika eneo la Magharibi Mkuu huyo wa mawaziri alionekana kubadilika kutoka mwanasiasa mpole hadi kutumia maneno makali.
Haya yalidhihirika alipowashambulia vikali aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka waliohoji chanzo cha fedha zilizotolewa kama marupurupu kwa wakulima wa miwa eneo la Mumias.
Bw Mudavadi atakuwa akikita kambi haswa katika kaunti anakotoka ya Vihiga akivumisha serikali ya Rais Ruto kupitia uzinduzi wa miradi na mipango ya maendeleo.
Kwa upande wake, Bw Wetang’ula, ametwikwa kibarua cha kukabiliana na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya na kiongozi wa chama cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-K) Eugene Wamalwa. Wawili hao ni wakosoaji wakuu wa Rais Ruto katika kaunti za Trans Nzoia na Bungoma, mtawalia.
“Siasa zinabadilika pakubwa nchini kiasi kwamba watu kama Joho na wanasiasa wengi kutoka Pwani wameamua kufanyakazi na Ruto. Majirani zetu, Bw Wandayi na Waluo wameamu kufuata mkondo huo, kwa hivyo tusiachwe nyuma. Pamoja na Oparanya, Musalia, Otuoma, Wako, na Wabunge wengine, sharti tuweke kando tofauti zetu na tuongee lugha moja huku tukiheshimiana kwa manufaa ya watu wetu,” Bw Wetang’ula akasema juzi wakati wa ziara ya rais katika eneo la Magharibi.
Kwa kuwa anao ufuasi mkubwa katika kaunti ya Bungoma, Bw Wetang’ula, akisaidiana na Gavana Kenneth Lusaka na Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa kudhibiti sio Mbw Natembeya na Wamwala, bali pia Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna.
Seneta Sifuna ambaye ni Katibu Mkuu wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) ameamua kukaidi msimamo wa viongozi wengine wa chama hicho kwa kupinga serikali ya Rais Ruto.
Katika kaunti ya Kakamega Waziri wa Ustawi wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya ndiye ataongoza kampeni ya kumvumisha Rais Ruto akisaidiana na gavana wa sasa wa Kakemega Fernandes Barasa.
Kutoka na tajriba yake ya zaidi ya miaka 25 katika siasa, ikijumuisha miaka 10 kama Mbunge wa Butere na miaka 10 kama Gavana wa Kakamega, Bw Oparanya anachukuliwa kama atakayefaidi Rais Ruto.
“Nimekuwa na Raila na sasa niko katika serikali hii jumuishi. Naomba tuungane kama ndugu kutoka eneo hili na tuunge mkono serikali,” Bw Oparanya akasema.
Alieleza kuwa ziara ya Rais hivi majuzi katika eneo la magharibi litafanikisha utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo huku Gavana Barasa akimhakikishia Dkt Ruto kwamba wakazi wa Kakamega watamuunga mkono katika uchaguzi wa 2027.
“Mheshimiwa Rais, usijali, tatuhakikisha kuwa wewe ndiwe unatamba hapa Kakamega,” Gavana Barasa.
Rais Ruto pia atamtegemea Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Nchini (COTU) Francis Atwoli kumsaidia kupata kura kaunti hiyo.
Katika kaunti ya Busia Rais anatarajiwa kutegemea usaidizi kutoka kwa Gavana Paul Otuoma na Balozi wa Maalum wa Kenya katika Umoja wa Mataifa (UN) na mbunge wa zamani wa Budalangi Ababu Namwamba
Leave a Reply