Kilimo kifanywe kwa mifumo ya kidijitali kuvutia vijana – Taifa Leo


SERIKALI na wadau husika katika sekta ya kilimo wametakiwa kuharakisha juhudi za kuweka mifumo ya kidijitali, ili kuvutia vijana.

Ikiwa matumizi ya teknolojia na bunifu za kisasa yatafanikishwa kikamilifu, vijana watavutiwa kushiriki kilimo, hivyo kupiga jeki ajenda ya uzalishaji chakula, kuangazia usalama na baa la njaa.

Wito huu umetolewa wakati ambapo washirika katika mtandao wa kilimo na chakula wanaelezea hofu yao kuhusu ushiriki mdogo wa vijana kwenye kilimo.

Kijana ambaye amekumbatia mfumo wa kidijitali kutoa mafunzo ya ufugaji. PICHA|SAMMY WAWERU

Kulingana na Prof Stephen Wambugu, Mkuu wa Kitivo cha Sayansi ya Jamii katika Chuo Kikuu cha Chuka, Tharaka Nithi, mifumo ya kidijitali ndio mbinu bora kuvutia vijana kushiriki shughuli za kilimo.

“Kizazi cha sasa—Gen Z na milenia, hawapendezwi na kazi za kilimo zinazohitaji kuchafuka mikono na za sulubu. Tukifanya kilimo kiwe cha kisasa, watafurika na kusaidia kuzalisha chakula,” anasema Prof Wambugu.

Anaeleza kuwa vijana wa kizazi cha sasa wanaona kilimo cha asili kuwa kazi ngumu na inayowachosha.

Prof Stephen Wambugu, Mkuu wa Kitivo cha Sayansi ya Jamii katika Chuo Kikuu cha Chuka, Tharaka Nithi akielezea kuhusu tija za mfumo wa kidijitali kuboresha sekta ya kilimo. PICHA|SAMMY WAWERU

Kupitia safu ya maendeleo ya teknolojia na uvumbuzi, vijana wanaweza kushiriki kilimo kupitia vifaa kama vile simu za mkono (rununu), tarakilishi ya kupakata, na kompyuta ili kutoa huduma kama ushauri nasaha kwenye kilimo na jinsi ya kuboresha bidhaa.

“Usiwaambie waamke saa kumi na moja alfajiri wakame ng’ombe au walime mashamba kwa jembe kama ilivyokuwa miaka ya sitini na sabini, hawatakubali. Tunahitaji kufanya kilimo kivutie zaidi kwa kukumbatia teknolojia,” anashauri Prof Wambugu.

Licha ya hamu yao kushiriki katika kilimo cha kisasa, vijana wanakumbwa na changamoto kadhaa, ikiwemo ukosefu wa dhamana kuomba mikopo kwenye mashirika ya kifedha.

Wengi wao hawana hatimiliki ya ardhi, hivyo basi kukosa namna ya kuinuka.

Apu ya kidijitali kutoa huduma za kilimo na ufugaji. PICHA|SAMMY WAWERU

 



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*