HATUA ya kutia nguvu muungano wa jamii za eneo la Mlima Kenya- Gikuyu, Embu na Meru (GEMA )- kwa kujumuisha Akamba, huenda ikawa mwiba kwa Kenya Kwanza na wakati huo huo kugawanya nchi kati ya maeneo mawili ya kukabiliana kisiasa iwapo chama cha ODM kitaunga Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu ujao.
Rais William Ruto alipata zaidi ya kura 4 milioni kutoka eneo la Mlima Kenya bila kaunti tatu za Ukambani za Machakos, Kitui na Makueni ambazo zilizo na karibu wapikura 2 milioni waliosajiliwa zilimuunga Bw Odinga aliyepeperusha bendera ya Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya.
Baada ya Rigathi Gachagua ambaye alikuwa mgombea mwenza wa Rais Ruto kuondolewa mamlakani kama Naibu Rais, dalili zinaonyesha kuwa eneo la Mlima Kenya limemtema Rais Ruto kisiasa huku akianza ukuruba wake na Bw Odinga aliyekuwa mpinzani wake mkuu katika uchaguzi wa 2022.
Serikali Jumuishi
Tayari, wanachama wa ODM ambao aliteua mawaziri chini ya Serikali Jumuishi wakiongozwa na aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho cha Chungwa John Mbadi (waziri wa Fedha) wanaunga Dkt Ruto kwa muhula wa pili iwapo Bw Odinga hatakuwa kwenye debe.
Bw Odinga anagombea wadhifa wa mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika na Rais Ruto anamuunga mkono.Wadadisi wa kisiasa wanasema GEMA mpya iliyozinduliwa Jumatano wiki hii, kuleta pamoja jamii za Mlima Kenya na Mashiriki mwa nchi inaweka msingi wa hali itakavyokuwa katika uchaguzi mkuu wa 2027 huku Dkt Ruto akikabiliwa na hatari ya kukosa zaidi ya kura 4 milioni alizopata mlimani alipogombea na Gachagua.
Ni hatua ya watu wenye ushawishi kutoka eneo la Mlima Kenya na Mashariki kuunga mkono mpango wa Gema mpya inayoufanya kuwa mwiba kwa mrengo wa Dkt Ruto na Bw Odinga.
Katika hatua ambayo huenda ikasababisha mabadiliko ya kisiasa katika siku zijazo, viongozi waliozungumza wakati wa hafla ya kuzindua Gema mpya walitoa wito wa umoja wa wakazi wa maeneo hayo yaliyo na wapigakura wengi.
Kuna dalili kwamba huenda muungano huo ukamuunga mkono kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka kugombea urais dhidi ya Rais Ruto na mrengo wake ambao huenda ukajumuisha chama cha ODM na hata Bw Odinga iwapo hatashinda uchaguzi wa mwenyekiti wa AUC.
Viongozi wa kijamii
Wazungumzaji waliojumuisha viongozi wa kidini, wazee na viongozi wa jamii, walisema wakati umefika kwa jamii za GEMA kumuunga mkono Kalonzo kumrudishia mkono kwa kumuunga aliyekuwa rais Mwai Kibaki alipokuwa akihitaji kuungwa mkono baada ya mzozo wa kisiasa wa 2007.Mzozo huo ulihusu chama cha ODM cha Bw Odinga na Party of National Unity ( PNU) cha Kibaki.
Mwaka huo, Rais William Ruto na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi walikuwa na Bw Odinga katika ODM huku Bw Musyoka akiongoza chama chake wakati huo kikifahamika ODM- Kenya.Ghasia zilipolipuka baada ya uchaguzi wa 2007, Bw Musyoka alijiunga na Kibaki na akateuliwa makamu rais.
Katika hafla ya kuzindua GEMA mpya viongozi waliozungumza waliashiria kwamba wanalenga mwelekeo mpya wa kisiasa.
Wachanganuzi wa siasa wanasema kuwepo kwa mjomba wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, George Muhoho, ambaye alihudumu kama waziri katika serikali ya Moi na mshirika wa karibu wa rais wa tatu wa Kenya Mwai Kibaki miongoni mwa watu wengine wenye ushawishi mlimani kunafanya muungano huo kuwa mwiba kwa ushirika wa Ruto na Odinga.
Mipango inaiva
Baadhi ya washirika wa karibu wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua pia walihudhuria mkutano huo.Mshirika wa karibu wa Kalonzo, Seneta wa Makueni Dan Maanzo baadaye alinukuliwa akisema kwamba mipango iko mbioni kuunda muungano thabiti unaoleta pamoja jamii zote za GEMA.
“Huu ni mwanzo wa kuundwa kwa muungano imara na utakauondoa utawala wa sasa. Jamii nyingine nyingi nje ya GEMA pia zitajiunga,” Maanzo alisema.Afisa wa utawala wa miaka mingi, Joseph Kaguthi.alisema GEMA inaunga mkono muungano unaojumuisha wote ambao unalenga kushughulikia matatizo ambayo Wakenya wamekuwa wakishughulikia.
“Kuna uwezekano wa kuibuka miungano miwili mikubwa ya Magharibi, Rift Valley na Nyanza kwa upande mmoja na mwingne wa Mlima Kenya na Mashariki mwa nchi,” asema mchambuzi wa siasa, Dkt Isaac Gichuki.
Anasema iwapo muungano kama huo utaiva na kudumu hadi 2027, uchaguzi wa mwaka huo utakuwa wenye ushindani mkubwa.
Leave a Reply