WANGECHI Muchiri alionyesha ustadi mkubwa akitawala mashindano ya ulengaji shabaha wa kutumia bastola ya Pink Target All Ladies Charity eneo la Kirigiti katika Kaunti ya Kiambu, wikendi.
Mashindano hayo ya siku moja yaliandaliwa Jumapili, Desemba 09, 2024 katika uga wa Chama cha kitaifa cha Wamiliki wa Bastola (NGAO) wa Kenya Shooting Range kwa lengo la kusherehekea wanawake na pia kuhamasisha kuhusu dhuluma za kijinsia. Wanawake pia walishiriki mashindano hayo ya ulengaji shabaha.
Wangechi alikamata nafasi ya kwanza kwa alama 99.77 kutoka orodha ya washiriki 68. Alifuatwa kwa karibu na Elizabeth Cherono (103.32), Silvia Kinya (110.58), Irene Ndunda (127.18), Agatha Muchiri (138.95), Brenda Ajiambo (143.51), Judy Wanja (144.22), Emmaculate Jepkosgei (161.88), Elizabeth Wachianga (169.80) na Sharon Langat (170.30) katika nafasi 10 za kwanza, mtawalia.
Mshauri wa Rais kuhusu masuala ya watoto na wanawake, Harriette Chiggai, aliyekuwa mgeni wa heshima, pia alipata mafunzo ya mchezo huo na hata kuujaribu.
Chiggai ameyarai makundi mbalimbali ya wanawake yashiriki miradi inayowainua ili kukabili changamoto zinazowaandama katika jamii.
Chiggai amesema kuwa siku 16 ambazo ni za uanaharakati kuhusu haki na kutokomeza dhuluma za kijinsia, zinastahili zitumike kuwazia jinsi ambavyo wanawake watajiinua na kufanikiwa maishani.
Kumekuwa na vifo 97 vinavyotokana na dhuluma za kijinsia na Chiggai anasema kuwa wale ambao wamelengwa sana ni wanawake na wasichana matineja.
“Haya mauaji yanastahili yakome kwa sababu hayasawiri kabisa utu na heshima kwa uhai wa binadamu. Hali hii inazua wasiwasi kuhusu usalama wa wasichana na watoto wetu nyumbani,” akasema Chiggai.
Akaongeza: “Kila mtu lazima ashiriki juhudi za kupata suluhu kwa suala hili. Kanisa lina jukumu, spoti ina wajibu na kama jamii, lazima tufanye wajibu wetu kuhakikisha wanawake hawahofii usalama wao na kuuawa kinyama.”
Hamasisho
Alishukuru kila mtu ambaye amejitokeza kuzungumzia mauaji ya wanawake ambayo yamekuwa yakiripotiwa huku akisema ni wanawake tu ndio watasababisha baadhi ya wanaume katili wabadilike.
Aidha, aliongeza kuwa baadhi ya mauaji hayo yanatokana na tamaduni na fikira potovu za kiakili kuhusu nafasi ya wanawake katika jamii. Wakati huu ambapo shule zimefungwa, Chiggai alishauri wazazi wamakinikie malezi ya watoto wao ambayo kwa sehemu kubwa hufanywa na walimu wakiwa shuleni.
Mashindano hayo ya ulengaji shabaha yaliyowaleta pamoja wanawake kutoka idara mbalimbali za serikali na sekta ya kibinafsi yaliandaliwa na Paula Munyi ambaye ni mwanzilishi wa kundi la wanawake wanaoshiriki ulengaji shabaha maarufu kama Pink Target Ladies Sports Shooting Club.
“Mwaka jana tuliandaa hamasisho kuhusu kansa ya matiti na mwaka huu ni kuhusu dhuluma ya kijinsia. Huwa tunatumia mchezo huu kuja pamoja kama wanawake kusaidia kupambana na changamoto mbalimbali za kijamii,” akasema Munyi.
Leave a Reply