NI afueni kwa zaidi ya maskwota 3,500 katika eneo la Taveta, Kaunti ya Taita Taveta ambao wamekuwa wakingoja hati miliki za mashamba yao kwa miaka nyingi baada ya serikali kuwapa stakabadhi za ardhi wanazoishi.
Akiongea Jumanne, Januari 14, 2025 kwenye hafla ya kuwakabidhi wakaazi stakabadhi hizo, Naibu Rais Bw Kithure Kindiki aliwahakikishia wakazi kuwa serikali itaendelea kutoa stakabadhi hizo katika maeneo mbalimbali nchini.
Bw Kindiki aliwahakikishia wakaazi wa maeneo hayo kuwa serikali inafanya kila juhudi kuhakikisha kuwa suala la migogoro ya ardhi katika kaunti hiyo linapata suluhu la kudumu.
Alitoa hati miliki hizo kwa maskwota wa maeneo ya Njukini na Eldoro.
Aidha, naibu Rais alisema kuwa afisi mbili za usajili wa ardhi zitafunguliwa mjini Voi na mjini Taveta ili kupunguza safari za kutafuta huduma katika afisi ta Ardhi iliyoko katika eneo la Wundanyi.
Bw Kindiki alisema kuwa dhamira ya serikali ni kuona wananchi wananufaika na rasilimali zilizopo ikiwemo ardhi.
Alisema kuwa serikali itahakikisha kuwa shamba lenye utata la Machungwani litarejeshwa kwa wakulima.
“Ninawahakikishia kwa niaba ya serikali tutatatua shida hii na shamba hili litarudi kwa wananchi wa Taita Taveta,” alisema.
Katibu wa Ardhi Bw Nixon Korir alisema kuwa katika maeneo mengi nchini bado wananchi wanaishi kama maskwota.
Alisema zaidi ya asilimia 60 ya ardhi nchini bado haina stakabadhi za umiliki wa ardhi.
“Hii inamaanisha kuwa ni asilimia 40 ya Wakenya ndio wako na vyeti vya umiliki wa ardhi zao. Ndio maana serikali inajikakamua kuhakikisha kuwa kila Mkenya anapata stakabadhi hii na ajiendeleze kimaisha,” alisema.
Katibu huyo alisema kuwa hati miliki 200,000 ziko tayari.
Katika kaunti ya Taita Taveta, alisema kuwa serikali inashughulikia hati miliki za maeneo matano.
“Zile hati miliki tuko nazo na ambazo zimechukua miaka nyingi zinashughulikiwa kwa mwezi mmoja ujao ili kiwawawezesha kuchangia katika kujenga uchumi na kuzalisha ajira.
Wananchi wa maeneo hayo ya Njukini na Eldoro walisema kuwa watatumia hati miliki hizo za ardhi kujikwamua kiuchumi
Wakiongea na Taifa Leo, walisema kuwa watatumia hati miliki zao kujiletea maendeleo ili kujenga uchumi wa eneo hilo.
Mwenyekiti wa chama cha ushirika cha wakulima wa Njukini Bw Timothy Nyambu alisema wamengoja vyeti hivyo kwa miaka nyingi na kuwa na wasiwasi kuhusu kufurushwa katika ardhi zao.
“Hati miliki za ardhi tulizopata ni mtaji hivyo titazitumia katika kujiendeleza kwa kuanzisha shughuli za uzalishaji kupitia mikopo kutoka katika taasisi za fedha kama mabenki ambayo yemeonesha dhahiri kuwa yako tayari kutukopesha kwa kutumia hati hizi,” alisema.
Leave a Reply