NAIBU Rais Kithure Kindiki amemuonya mtangulizi wake Rigathi Gachagua kwa kuwachochea Wakenya dhidi ya serikali.Katika taarifa yenye maneno makali, Prof Kindiki alionya kuwa, Gachagua hataruhusiwa kujihusisha na shughuli za kisiasa ambazo zinaweza kusababisha uharibifu nchini.
Akizungumza jana katika Kanisa la Kamumu Full Gospel katika eneo la Mbeere kaunti ya Embu, Prof Kindiki alimshutumu Bw Gachagua kwa kusema uongo kila mara kuhusu serikali na kuwadharau viongozi wengine.
Naibu Rais alimshutumu Gachagua kwa kubuni uongo kwamba, serikali haijaanzisha miradi yoyote ya maendeleo yenye manufaa kwa Wakenya katika kipindi cha miaka miwili ambayo imekuwa mamlakani lakini hakuwa akitoa suluhu.
“Katika nchi hii, hatutaruhusu mtu yeyote kuzunguka nchi nzima kuwachochea Wakenya bila kuwasaidia kutatua matatizo yao. Hatutaruhusu hili kuendelea,”alisema akimrejelea Bw Gachagua.
Wakati huo huo, alimwambia Bw Gachagua kuwaheshimu viongozi wanaoshirikiana na serikali.
“Mimi sio mwoga, tunastahili kuheshimiwa. Nilipokuwa Waziri wa Masuala ya Ndani, majangili waliokuwa wakiiba ng’ombe na kuua watu walinidharau. Walitembea huku na huko wakisema singeshinda vita dhidi ya ujangili. Niliwathibitishia kuwa mimi sio wa kuchezea,” alisema.
Alimkashifu Bw Gachagua kwa kuwarushia matusi wabunge wa Mlima Kenya baada ya kutofautiana nao kufuatia kutimuliwa kwake.
“Ni makosa kuwadharau Wabunge. Ikiwa wabunge walikosea, alipaswa kuwarekebisha kwa njia ya kistaarabu,” alisema. Hata hivyo, Bw Kindiki aliwashauri viongozi kote nchini kukoma kuvuruga mikutano ya kisiasa ya wapinzani wao.
“Nitashutumu mtu yeyote anayelipa wahuni ili kusababisha fujo kwenye mikutano,” alisema.Prof Kindiki alikariri kuwa Mlima Kenya ni eneo moja na akawataka wakazi kupinga majaribio ya kuligawanya mara mbili- Mashariki na Magharibi.
“Sisi ni watu wa jamii moja na tunapaswa kuendelea kuwa pamoja ili tunufaike na miradi ya maendeleo inayofanywa na Serikali.Wabunge kutoka Mlima Kenya Geoffrey Ruku (Mbeere Kaskazini), Nebart Muriuki (Mbeere Kusini), Eric Wamumbi (Mathira) Patrick Munene (Chuka- Igambang’ombe) na Gitonga Murugara wa Tharaka walimkemea Bw Gachagua, na kumkumbusha kwamba wako serikalini na hawataondoka. Walisema hakuna vitisho vyovyote ambavyo vitawafanya kujitenga na serikali.
Wabunge hao walishangaa jinsi Gachagua anatarajia maeneo yao kupata maendeleo bila kuungwa mkono na serikali.
“Tunataka maeneo bunge yetu yawe na barabara nzuri, umeme na maji ya unyunyiziaji kwa watu wetu na lazima tubaki serikalini. Tunamuunga mkono kikamilifu Rais William Ruto na Naibu wake Kindiki,” alisema Bw Ruku.
Wabunge hao walimwambia Bw Gachagua akome kuwahujumu au akabiliane na ghadhabu zao.“Tulichaguliwa na wananchi na Bw Gachagua anafaa kutuheshimu,” akasema Bw Munene.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA
Leave a Reply