JUMUIYA ya Afrika Mashariki inashirikisha nchi nane wanachama: Kenya, Uganda na Tanzania ndio wanachama waasisi. Kisha kuna Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Somalia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (JKK).
Chombo kikuu cha Jumuiya ni Mkutano wa Marais wa mataifa hayo. Kikao cha 24 cha viongozi hao wa nchi kilifanyika mwezi jana jijini Arusha, Tanzania chini ya uenyekiti wa Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir Mayardit.
Katika wasilisho kwa vyombo vya habari mnamo tarehe 30 Novemba, kikao kiliorodhesha hoja kumi na sita. Hoja ya sita ilieleza kuwa viongozi hao walipitisha na kutia saini hoja kwamba marekebisho yafanywe kwenye Ibara ya 137 ya mkataba ulioasisi Jumuiya ili kutambua Kiswahili na Kifaransa kama lugha rasmi za Jumuiya baada ya Kiingereza. Kwa sababu hiyo, Kiswahili kitatumiwa katika vyombo na asasi zote za Jumuiya.
Japo kumekuwa na tetesi kuwa haikufaa kuteua lugha nyingine ya kigeni kuwa rasmi, nafikiri ni muhimu kuelewa hali halisi ya kisiasa na kimawasiliano inayokabli mataifa husika.
Uteuzi wa Kiswahili na Kiingereza pekee utasababisha changamoto kwa baadhi ya mataifa kama vile Burundi na JKK. Tunafaa kuona hatua muhimu ya uteuzi wa Kiswahili na kujitahidi kukikuza na kukipatia mashiko zaidi katika Jumuiya ili kiweze kushika usukani kihalisia bila kushinikizwa.
Hatua iliyochukuliwa na marais ni muhimu na inafaa kupongezwa. Hata hivyo, hili lisiwe tamko tu, wawe mstari wa mbele kupigia debe Kiswahili. Mkataba wa Jumuiya unashinikiza nchi wanachama kuunda mabaraza ya Kiswahili.
Nchini Kenya, bado twasubiri. Kwa kuwa Rais William Ruto aliteuliwa Mwenyekiti wa Jumuiya, nafikiri ataongoza kwa hili.
Leave a Reply