Kocha mgeni wa Gor Mahia kujaribiwa Dandora, Police na Tusker zikipigania kileleni KPL – Taifa Leo


MBIVU na mbichi itabainika wikendi hii wakati ambapo Viongozi wa Ligi Kuu (KPL) Kenya Police watapambana na Tusker kwenye mechi kali katika uga wa Kenyatta, Kaunti ya Machakos mnamo Jumamosi.

Mabingwa watetezi Gor Mahia ambao ni nambari tatu nao watamkaribisha kocha wao mpya raia wa Croatia Sinisa Mihic wakiwa wageni wa Mathare United katika uga wa Dandora, Kaunti ya Nairobi. Mechi hiyo pia itagarazwa Jumamosi na itakuwa ya kwanza kwa kocha huyo aliyetambulishwa Jumatatu wiki hii.

AFC Leopards ambao ni mabingwa mara 12 nao watakuwa wenyeji wa Kariobangi Sharks katika uga wa Dandora mnamo Jumapili. Ingwe inashikilia nafasi ya nne kwa alama 29 baada ya mechi 18.

Mtanange kati ya Kenya Police na Tusker utakuwa wenye mtihani mkali kwa sababu timu zote zina alama 37 baada ya mechi 19.

KPL itakuwa ikiingia raundi ya 20 wikendi hii mechi nne zikichezwa Jumamosi na nyingine tano siku ya Jumapili.

Kenya Police imekuwa moto wa kuotea mbali na imecheza mechi 11 bila kushindwa tangu Disemba 1. Kocha wa Police raia wa Burundi Etienne Ndayiragije ambaye alijiunga na timu hiyo Novemba 29 ameinua kikosi hicho kutoka nafasi ya kushushwa ngazi hadi kileleni mwa KPL.

Tusker pia inaonekana imeimarika chini ya kocha Charles Okere ambapo hawajashindwa katika mechi nne zilizopita. Okere atakuwa akimtegemea Ryan Ogam ambaye amefunga mabao 15 kwenye mechi 17 na hakuhamia Algeria jinsi ilivyotarajiwa wikendi iliyopita.

Kenya Police nao wamepiga jeki kikosi chao kipindi hiki cha uhamisho wa wanasoka kwa kumnunua straika mkali wa Nairobi City Stars Mohamed Bajaber.

Tusker na Kenya Police zimecheza mara saba, Tusker ikishinda mara tatu, Kenya Police mara moja kisha mechi tatu zimeishia sare. Sare kati ya timu hizi zitakuwa pigo kwao hasa iwapo Gor itaibwaga Mathare United Jumamosi.

K’Ogalo  ina alama 31 baada ya kusakata mechi 18 na iwapo itashinda mechi hiyo ya ziada itajiweka pazuri kutetea ubingwa wake wa 22.

Wakati huo huo, Shabana imekamilisha usajili wa wachezaji watatu kutoka kwa klabu pinzani ya KPL.

Klabu hiyo imezinasa huduma za mshambuliaji Moses Shikanda na kiungo matata Keith Imbali, ambao wote wamejiunga nao kutoka Kariobangi Sharks.

Tore Bobe pia imepata huduma za kiungo mwingine, Douglas Mokaya kutoka Bidco United, huku ikilenga kuendeleza matokeo mazuri ya sasa baada ya mwanzo mbaya wa msimu.

Tangu Kocha Peter Okidi achukue usukani Novemba mwaka jana, ameisaidia Shabana kupanda kutoka eneo hatari hadi nafasi yake ya saba kwa pointi 28.

RATIBA

JUMAMOSI

Tusker v Kenya Police (Kenyatta, Machakos, 4pm)

Bidco United v Nairobi City Stars (Kenyatta, Machakos, 1pm)

Bandari v Sofapaka (Mbaraki, Mombasa, 3pm)

Mathare United v Gor Mahia (Dandora, Nairobi, 4pm)

JUMAPILI

Mara Sugar v FC Talanta (Awendo, Migori, 3pm)

Posta Rangers v Shabana (Kenyatta, Machakos, 4pm)

KCB v Murang’a Seal (Kenyatta, Machakos, 1pm)

AFC Leopards v Kariobangi Sharks (Dandora, Nairobi, 4pm)

Ulinzi Stars v Kakamega Homeboyz (Dandora, Nairobi, 1pm)

 



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*