
JAJI MKUU Martha Koome na Jaji wa Mahakama ya Juu Njoki Ndung’u wameelekea katika Mahakama Kuu kuzuia kuondolewa kwao afisini kutokana na pendekezo la aliyekuwa Waziri Raphael Tuju na wakili Nelson Havi.
Jaji Koome anataka agizo la kuzuia Tume ya Huduma za Bunge (JSC) kuanza mchakato wa kumtimua, akisema kuna uwezekano wa mapendekezo kuwasilishwa kwa Rais kuunda jopo la kumchunguza na hivyo basi kukiuka na kumnyima haki.
Katika stakabadhi zilizowasilishwa mahakamani na wakili Andrew Musangi, Jaji Ndung’u amewasilisha kesi dhidi ya JSC akisema mchakato unaoendelea hapo huenda ukaishia kuondolewa kwake afisini na kuundwa kwa jopo la kuchunguza mienendo yake na majaji wenzake wa Mahakama ya Juu.
Anataka JSC izuiliwe kushughulikia maombi yaliyowasilishwa dhidi yake na majaji wengine sita wa mahakama hiyo, akiwemo Jaji Mkuu KoomeJapo JSC inashughulikia maombi matatu yaliyowasilishwa na kampuni ya Dari Limited inayomilikiwa na Bw Tuju, Bw Havi na wakili Christophet Rosan, stakabadhi za mahakama zinaonyesha kuwa Jaji Njoki hapingi ombi lililowasilishwa na mlalamishi wa tatu.
Bw Tuju na Bw Havi pamoja na Bw Rosana wameitaka JSC iwafute kazi majaji wote saba wa Mahakama ya Juu kwa utendakazi mbaya na utovu wa maadili walipokuwa wakishughulikia kesi mbalimbali.
Jaji Njoki anataka Mahakama Kuu iamuru kusitishwa kwa JSC kushughulikia maombi hayo hadi kesi aliyoiwasilisha itakapoamuliwa.Anataja mchakato unaoendelezwa kwa nia ya kumwondoa afisini kama “unaokiuka katiba na usio na msingi wowote.”
Jaji Njoki anaeleza kuwa shughuli zinazoendelea katika JSC kuhusiana na maombi hayo zinahalalisha mamlaka ya majaji ya kutoa maamuzi na hivyo ni kinyume cha kipengele cha 160 cha Katiba kinacholinda uhuru wa Idara ya Mahakama.
Aidha, Jaji hiyo anaamini kuwa hatua ya JSC inakwenda kinyume na kanuni ya kuwalinda majaji kutokana na kuingiliwa bila sababu.Jaji Ndung’u pia alikosoa JSC kwa kupokea maombi hayo na kuyaorodhesha kusikizwa, akisema hilo likiruhusiwa kuendelea “watu wenye nia mbaya wataendelea kutumia JSC kama silaha za kuwasaidia kuendesha vita dhidi ya majaji kufanikisha malengo yao finyu.

.“Huku Jaji Njoki akitambua na kuheshimu wajibu wa JSC katika kuendeleza uwajibikaji katika idara ya mahakama, ni wazi kuwa wajibu huo haujumuishi kubatilisha maamuzi ya majaji yanayotolewa wanapotekeleza majukumu yao,” akasema wakili Musangi.
Mnamo Alhamisi, wakili Nelson Havi alikata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu ya Narok wa kusitisha mchakato wa kuwaondoa majaji saba wa Mahakama ya Juu. Wakili Nelson Havi alisema mchakato wa kikatiba hauwezi kusitishwa kwa maagizo ya muda.Anasema hiyo ni sawa na kusitisha kipengele cha katiba na kuzuia Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) kufanya kazi yake.
Bw Havi aliikosoa kesi iliyowasilishwa na Bw Pariken ole Esho, kupinga uamuzi wa JSC wa kuwataka majaji kujibu shutuma zinazowakabili. Alieleza kusikitishwa na maagizo ya muda yaliyotolewa na Jaji Charles Kariuki Jumatano kuzuia JSC kuendelea na malalamishi matatu ya kuwaondoa afisini majaji hao wa mahakama ya juu kwa madai ya utepetevu na utovu wa nidhamu.
Maagizo hayo yataendelea kutumika hadi kuamuliwa kwa kesi iliyowasilishwa na Bw Ole Esho. Kulingana Bw Havi katika kesi yake majaji saba wa Mahakama ya Juu hawakuwa wamepinga agizo la kujibu kesi ya kuondolewa kwao.
Leave a Reply