HUKU kampeni za uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) zikielekea katika mkondo wa lala-salama, mtazamo kuwa kiongozi wa Upinzani nchini Raila Odinga aling’ara kwenye ‘Mjadala Afrika’ unapiga jeki nafasi yake katika kinyang’anyiro hicho cha bara Afrika.
Bw Odinga alikumbana na mpinzani wake mkuu, Waziri wa Masuala ya Nje wa Djibouti Mahmoud Ali Youssouf na Richard Randriamandrato wa Madagascar kwenye mjadala huo uliofuatiliwa na watu mbalimbali barani.
Mdahalo huo uliandaliwa katika makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU) jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Bw Javas Bigambo anasema kuwa japo Wakenya wamekuwa na maoni mseto kuhusu jinsi mjadala huo ulivyoendelea, Bw Odinga alidhihirisha ufahamu mkubwa wa masuala ya Afrika kuliko wapinzani wake.
Bw Bigambo anasema Raila alifanya vyema kwenye Mjadala Afrika kuliko mshindani wake mkuu Bw Youssouf ila hilo si hakikisho kuwa ameshinda kura hiyo.
“Baba alitoa ufafanuzi wa kuridhisha kuhusu historia ya Afrika, malengo ya Afrika na ushirikiano katika kulinda rasilimali na jinsi ya kutumia rasilimali hizo,” akasema Bw Bigambo
“Youssouf naye alikuwa wembe hasa kuhusu masuala ya kidiplomasia. Kile Raila hakufanya ni kuorodhesha ufanisi wake alipokuwa mwakilishi wa Afrika kuhusu Masuala ya Miundomsingi,” akaongeza.
Kauli ya Bw Odinga kuwa iwapo atashinda kiti hicho atahakikisha Afrika ina wawakilishi wawili katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC), ilionekana kuchangamkiwa zaidi.
Akifanikiwa alisema kuwa sharti wawakilishi hao wawe na mamlaka ya kudumu kama wawakilishi wa Afrika.
Bw Odinga alilalamika kuwa Afrika ambayo ina nchi 55 haina hata mwakilishi mmoja katika baraza hilo ilhali bara Ulaya lina viti vitatu.
“Siendi kuzungumzia suala la mwakilishi wa kudumu. Iwapo marais wataona ni bora niwe mwenyekiti wa AUC, basi nitahakikisha tunapata uwakilishi sawa katika kiwango cha kimataifa,” akasema.
Viongozi kutoka mirengo mbalimbali ya kisiasa nchini walimpongeza Bw Raila wakisema aliwika kwenye mjadala huo.
Hata hivyo, wengine hasa kutokana na miegemeo yao ya kisiasa nchini, walisema hawaungi Bw Odinga huku wakimpigia chapuo Bw Youssouf kwa kiti hicho.
Mbunge wa zamani wa Nyeri Mjini Wambugu Ngunjiri ambaye ni mwandani wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, naye alichemka mtandaoni akionekana kutoridhishwa na jinsi Raila alivyojibu maswali aliyoulizwa.
“Kile ambacho kimejidhihirisha kwenye mjadala huu ni kuwa Raila huwa anataka sheria zibadilishwe kumpendelea,” akaandika Bw Ngunjiri mitandaoni.
Lakini mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi Herman Manyora anasema kwa sasa Raila anastahili kuungwa mkono na Wakenya wote badala ya tofauti za siasa za hapa nchini kutumiwa kumpiga vita.
“Badala ya kumtakia mabaya, yafaa tumuunge mkono. Raila alifanya vyema kwenye mjadala lakini kuna watu ambao wanaeneza propaganda na hata kumchafulia jina AUC kutokana na siasa zetu za hapa. Huo sio uzalendo,” akasema Bw Manyora.
Kauli ya Bw Manyora inalandana na ya Gavana wa Kisumu, Prof Anyang’ Nyong’o na mwenzake wa Nairobi, Johnson Sakaja.
“Nimeongea na rafiki zangu katika nyanja za kiakademia barani Afrika na wameniambia kuwa Raila alifanya vyema kwenye mjadala huo kuliko wapinzani wake,” akasema Prof Nyong’o ambaye ni kaimu kiongozi wa chama cha ODM.
“Kwa kuwa amefanya kazi AU kama Mjumbe wa Miundomsingi, Raila alionyesha kweli kuwa anafahamu masuala ya bara hili na hata kupendekeza kile ambacho kinastahili kufanywa,” akaongeza.
Gavana Sakaja ambaye aliandamana na Bw Odinga kwenye ziara hiyo vilevile alifanana kimaoni na Prof Nyong’o.
“Hongera Baba. Kweli umeonyesha kuwa una ujuzi kuhsusu masuala ya Afrika, wewe ni kama kitabu cha historia na ulionyesha wakati wa mjadala kuwa wewe ni mwana wa Afrika,” akasema Bw Sakaja.
Mjadala huo umeibua matumaini miongoni mwa wafuasi wa Bw Raila nchini kuwa mara hii atafanikiwa kutwaa uenyekiti wa AUC baada ya kuanguka kura ya urais mara tano.
Bw Odinga amekuwa kwenye ziara za kampeni Magharibi, Kaskazini na Kusini mwa Afrika ambapo amekuwa akibisha katika milango ya ikulu baada ya kuhakikishiwa uungwaji mkono na mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Rais wa Nambia Adama Barrow ambaye alikuwa mgeni wa heshima nchini wakati wa maadhimisho ya Jamhuri Dei mnamo Alhamisi aliweka wazi kuwa taifa hilo litaunga mkono uwaniaji wa Raila.
Hata hivyo, kwa kuwa marais ndio hupiga kura, kuna vigezo vingi ambavyo vinaonyesha kuwa safari bado ndefu na huenda mjadala huo pekee ukakosa kutoa taswira kamili ya mshindi.
AU huwa na bajeti ambayo inafadhiliwa na Amerika na bara Ulaya kwa hivyo huenda wakashawishi marais kupiga kura kwa mkondo fulani hapo Februari 2025.
Mataifa kama Afrika Kusini yana uhusiano wa karibu na Urusi na huenda yakaamrishwa kupiga kura kwa mkondo fulani kulinda maslahi yake kiuchumi.
Suala la kidini pia huenda likaamua mwelekeo wa kura ambapo kambi ya Bw Odinga huenda ikakosa kura kutoka kwa nchi ambazo marais wazo ni Waislamu iwapo yataungana na yaamue kuunga mwaniaji wa Djibouti.
Leave a Reply