Kuondoa Karanja, Ndung’u uwaziri ishara Ruto anataka wanasiasa serikalini kuelekea 2027 – Taifa Leo


SIKU za wataalamu waliosalia katika baraza la mawaziri la mawaziri zinaonekana kuwa finyu baada ya Rais William Ruto kuendeleza mtindo wake kuwateua wanasiasa kuwa mawaziri akianza kujipanga kwa uchaguzi mkuu wa 2027.

Katika mabadiliko yaliyotangazwa Alhamisi, Desemba 19, 2024, Dkt Ruto amewaondoa mawaziri wawili wataalamu; Dkt Margaret Nyambura (ICT) na Dkt Andrew Karanja (Kilimo) na kupendekeza wanasiasa William Kabogo na Mutahi Kagwe, mtawalia, kuchukua nafasi zao.

Sasa mawaziri, wasio na tajriba ya kisiasa, waliosalia ni; Deborah Barasa (Afya), Eric Mugaa (Maji), Julius Migos Ogamba (Elimu) na Rebecca Miano (Utalii).

Japo Dkt Nyambura amehitimu kwa shahada ya Uzamifu katika taaluma ya teknolojia ya habari na mawasiliano na amefanyakazi katika sekta hiyo kwa miaka 26, Rais Ruto amemtema kwa sababu “hajakuwa akivumisha sera na mipango ya serikali moja kwa moja kwa wananchi katika ngazi za mashinani.”

Ndipo, Rais akampendekeza kuwa balozi wa Kenya nchini Ghana.

Dkt Ruto amempendekeza Bw Kabogo, ambaye ni gavana wa zamani wa Kiambu, kushikilia wadhifa wa Waziri wa ICT licha ya kwamba elimu yake na tajriba yake haziafiki majukumu ya wizara hiyo.

Bw Kabogo, ambaye pia amehudumu kama Mbunge wa Juja kwa mihula miwili (kati ya 2002 na 2013), amehitimu kwa Shahada ya Digrii ya Biashara kutoka Chuo Kikuu cha Punjab nchini India.

Naye Bw Kagwe, ambaye ni mwandani wa Rais wa mstaafu Uhuru Kenyatta, ameteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo kuchukua mahala pa Dkt Karanja, mtaalamu wa Kilimo mwenye tajriba ya miaka 36 katika sekta hiyo.

Bw Kagwe amehudumu kama Mbunge wa Mukurwe-in kati ya mwaka wa 2002 hadi 2007. Ni wakati huo ambapo Rais Kenyatta alimteua kuwa Waziri wa ICT, wadhifa alioushikilia kati ya 2006 na 2007.

Baada ya uchaguzi mkuu wa 2013, Kagwe alihudumu kama Seneta wa Nyeri hadi mwaka wa 2017.

Mnamo Februari 28, 2020 mwanasiasa huyo aliteuliwa Waziri wa Afya kuchukua mahala pa Bi Sicily Kariuki.

Ni wakati wa hatamu yake katika wizara hiyo ambapo aliongoza juhudi za serikali za kupambana na mlipuko wa ugonjwa Covid-19 kuanzia March 13, 2020 hadi 2022.

Akitangaza mabadiliko hayo katika baraza la mawaziri, ubalozi na usimamizi wa mashirika ya serikali, Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei aliyataja kama ambayo yanalenga kuimarisha utoaji huduma katika asasi husika.

“Teuzi hizo na mabadiliko ya majukumu yanaakisi kujitolea kwa Ras kulainisha na kuimarisha shughuli za serikali ili kuafiki mahitaji ya Wakenya,” Bw Koskei akaeleza.

Lakini kulingana na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Herman Manyora, kimsingi, Rais Ruto aliongozwa na msukumo wa kisiasa katika kufanya mabadiliko hayo bali sio nia ya kuimarisha utoaji huduma kwa wananchi alivyodai Bw Koskei.

“Kimsingi, Rais Ruto amewapendekeza wanasiasa kama vile Mutahi Kagwe, William Kabogo na Lee Kinyanjui kuwa mawaziri sio kwa lengo la kuimarisha utendakazi wa serikali yake bali nia yake ni kuwatumia kuokoa ushawishi wake katika eneo la Mlima Kenya. Watatu hao wameletwa kudhibiti mawimbi ya uasi dhidi ya Ruto katika Mlima Kenya yaliyochochewa na kuondolewa kwa Rigathi Gachagua kama Naibu Rais,” anaeleza.

“Wale ambao wamevuliwa nyadhifa za uwaziri kutoa nafasi kwa Mabw Kabogo na Kagwe, Dkt Nyambura na Dkt Karanja, wamekuwa wakitekeleza kazi moja tu ya uwaziri bali sio ili ya kumvumisha Rais Ruto kisiasa. Hii ndio maana wameonekana kutomfaa haswa eneo la Mlima Kenya wanakotoka,” Bw Manyora anaongeza.

Mhadhiri huyo wa Chuo Kikuu cha Nairobi anasema kuwa mwaka ujao, Rais Ruto ataweka kwenye “mizani ya kisiasa” thamani ya mawaziri wengine ambao sio wanasiasa ili kuamua ikiwa ataendelea kudumisha kwenya baraza lake au la.

Dkt Nyambura, Dkt Karanja na mawaziri Dkt Barasa, Dkt Muuga (Maji) na Bw Ogamba (Elimu) ni miongoni mwa mawaziri wasio wanasiasa walioteuliwa Julai mwaka huu Rais Ruto alipovunja baraza lake la mawaziri kufuatia maandamano ya Gen Z.

Ni wakati huo ambapo Dkt Ruto pia aliteua viongozi watano wa ODM kuwa mawaziri katika hatua iliyoonekana kulenga kutuliza uasi dhidi ya serikali yake.

Wao ni waliokuwa manaibu kiongozi wa ODM Ali Hassan Joho na Wycliffe Oparanya, aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho John Mbadi, aliyekuwa kiongozi wa wachache bungeni Opiyo Wandayi na aliyekuwa mwanachama wa Kamati ya Uchaguzi ya ODM, Beatrice Askul.

Tangu waingie afisini Mabw Joho, Mbadi, Oparanya na Wandayi wamekuwa mstari wa mbele kuipigia debe serikali ya Rais Ruto katika majukwaa mbalimbali ya kisiasa.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*