Lazima nikae karibu na Rais nitetee wafanyakazi, wala si kujinufaisha – Taifa Leo


KATIBU Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi Nchini (COTU) Francis Atwoli Jumapili alitetea ukuruba wake na serikali, akisema unalenga kuendeleza masilahi ya wafanyakazi.

Bw Atwoli alisema muungano huo umejitolea kuendeleza haki na masilahi ya wafanyakazi ambayo hufikiwa kupitia mazungumzo ambayo ndio mojawapo ya nguzo tatu za Shirika la Leba Ulimwenguni (ILO)

“Mazungumzo na wadau yanashirikisha majadiliano na serikali iliyoko mamlakani ili kuhakikisha kuwa masuala ya wafanyakazi yanashughulikiwa. Haya hayahusiani na siasa za kujitakia makuu au ya kuegemea mrengo mmoja bali njia za kulinda masilahi ya wafanyakazi,” Bw Atwoli akasema kupitia taarifa.

Alisema mafanikio ya Cotu yakiwemo kutetea mishahara bora, kuendeleza masilahi ya wafanyakazi na kuelekeza sera za leba ni vielelezo vya matunda ya utendakazi wa muungano huo.

Bw Atwoli alisema kama Katibu Mkuu wa Cotu, ataendelea kufanya mazungumzo ya serikali iliyoko mamlakani “kwa moyo wa ushirikiano.”

“Kujitolea kwetu kuimarisha maisha na masilahi ya wafanyakazi kunasalia imara,” akasema.

Alisema kanuni ya utatu, ilivyoelezwa katika sheria ya ILO, ni ile inayoleta pamoja wafanyakazi, waajiri na serikali katika kushughulikia masuala ya sekta ya leba kwa pamoja.

“Kama muungano wa vyama wa wafanyakazi, wajibu wetu sio kuendesha siasa za mapendeleo bali kutetea masilahi ya wafanyakazi. Na chombo cha kutumia katika utekezaji wa wajibu huo ni mazungumzo na wadau katika sekta ya leba,” akasema.

Mazungumzo kati ya Cotu, waajiri na wafanyakazi huhakikisha kuwa sauti za wafanyakazi zinasikika katika ngazi ya utengenezaji sera, yakiwezesha kushughulikiwa kwa malalamishi ya wafanyakazi na kufikiwa kwa malengo ya maendeleo.

Bw Atwoli, amelazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya baadhi ya vyombo vya habari kukosoa hatua yake ya kumkaribisha Rais William Ruto nyumbani kwake Khwisero, Kakamega wiki jana.

Aidha, kwa mara sio moja tangu Rais Ruto kuingia mamlakani mnamo Septemba 13, 2022, Bw Atwoli amehudhuria mikutano katika Ikulu ya Nairobi akiandamana na wanasiasa kutoka jamii ya Waluhya.

Lakini jana, kiongozi huyo wa Cotu, alisisitiza kuwa kinachomvutia kuhudhuria mikutano kama hiyo ni haja ya kutetea masilahi ya wafanyakazi wala sio kuwaidhinisha wanasiasa fulani.

Mfano mzuri ni kujitolea kwa Cotu kuendeleza masilahi ya wafanyakazi, Bw Atwoli anaeleza, ni kwa kuunga mkono kungezwa kwa makato ya Hazina ya Malipo ya Uzeeni (NSSF) na kuundwa kwa Mamlaka ya Afya ya Kijamii (SHA).

Japo, hatua hizo zimepingwa na raia Bw Atwoli amekuwa akizipigia debe akisema zinalinda masilahi na mustakabali wa wafanyakazi nchini Kenya.

“Tumeunga mkono kuongezwa kwa makato ya NSSF kwa imani kuwa wafanyakazi wanahitaji fedha za kujisaidia baada ya wao kustaafu,” Atwoli anasema.

Wakosoaji wamemsuta Atwoli kwa kuwa karibu sana na serikali na hivyo kufeli kutetea masilahi ya wafanyakazi.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*