MAAFISA 20 miongoni mwa 400 wa polisi wa Kenya wanaohudumu nchini Haiti kupambana na genge chini ya kikosi cha Umoja wa Mataifa, wamewasilisha barua za kujiuzulu katika kipindi cha miezi miwili iliyopita kwa sababu ya kucheleweshwa kwa malipo, maafisa watatu waliambia Reuters.
Maafisa hao hawajajibiwa barua zao na wanaendelea kuhudumu, walisema maafisa hao watatu, ambao waliomba kutotajwa majina yao kwa sababu hawakuruhusiwa kuzungumza na vyombo vya habari.
Msemaji wa polisi wa Kenya hakujibu simu na jumbe za kutaka maoni yake kuhusu barua za kujiuzulu kwa maafisa hao, ucheleweshaji wa malipo na mazingira ya kazi.
Mkuu wa polisi wa kitaifa Douglas Kanja alikanusha ripoti za ucheleweshaji wa malipo katika mkutano na wanahabari Jumatano, akisema maafisa hao walikuwa wamelipwa “hadi kufikia mwisho wa Oktoba”.
Maafisa hao watatu walipinga hili, wakisema walilipwa mara ya mwisho Septemba.
Kenya imetuma takriban maafisa 400 tangu Juni mwaka huu kuongoza kikosi cha kupambana na magenge nchini Haiti, ambacho kinapaswa kuwa na maafisa 2,500 kutoka takriban nchi 10, lakini kikosi hicho kinakabiliwa na tatizo la ufadhili.
Ni maafisa wachache tu kutoka mataifa mengine ambao wamewasili Haiti, na ahadi ya Rais wa Kenya William Ruto kutuma maafisa wengine 600 Novemba haikutimia.
Maafisa hao watatu waliambia Reuters kwamba wenzao walianza kuwasilisha barua za kujiuzulu Oktoba baada ya kujaribu kujiuzulu kwa maneno na kuambiwa wafanye hivyo kwa maandishi.
Maafisa watatu waliwasilisha barua za kujiuzulu mnamo Oktoba na wengine 15 au zaidi mnamo Novemba. Miongoni mwao ni kamanda wa kitengo, ambaye alikuwa wa kwanza kuwasilisha barua mwezi Oktoba, walisema.
Ghasia za magenge ambayo yameua maelfu ya watu kote Haiti katika kipindi cha miaka miwili iliyopita zimezidi kuwa mbaya hivi karibuni, huku makundi yenye silaha yakienea mwezi uliopita katika baadhi ya sehemu za mji mkuu m ambazo hazikuwa chini ya udhibiti wao.
Afisa mmoja alisema hakuwa amejitayarisha kwa yale aliyokumbana nayo Haiti na “amekuwa akiteswa na matukio kama mbwa wakila nyama ya binadamu barabarani”.
Maafisa hao pia walisema hawakuwa na risasi za kutosha kukabiliana na magenge hayo ambayo yamezidisha mashambulizi dhidi ya polisi wa Kenya.
Maafisa wanne waliiambia Reuters mnamo Septemba kwamba walikuwa wakicheleweshewa mishahara pamoja na kukumbwa na uhaba wa vifaa.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA
Leave a Reply