HALI tofauti kabisa inawasubiri wazazi, shule na biashara zinazoendeshwa katika sekta ya elimu, wanafunzi watakaporejea shuleni kwa muhula wa kwanza Jumatatu, Januari 6.
Kwa mara ya kwanza tangu 1985, hakutakuwa na usajili wa wanafunzi wa Kidato cha Kwanza 2025 huku mtaala wa CBC ukiingia awamu mpya baada ya mfumo wa awali wa 8-4-4 kuvunjiliwa mbali katika shule za msingi.Hakukuwa na usajili wa wanafunzi wa kidato cha kwanza 1985 baada ya muda wa elimu ya shule ya msingi kuongezewa kutoka miaka saba hadi minane, 8-4-4 ilipoanzishwa.
Darasa la Nane la mwisho liliondoka shule ya msingi 2023 ambapo 2024 hakukuwa na mitihani ya Darasa la Nane (KCPE).Kundi la kwanza la CBC litajiunga na Gredi 9, ambalo ni darasa la mwisho la sekondari ya msingi iliyopo katika shule za msingi.
Kutokana na hali hii, shule za sekondari zinatazamiwa kupoteza mabilioni ya fedha ambazo zimekuwa zikipokea chini ya mpango wa Elimu ya Kutwa ya Sekondari Bila Malipo (FDSE) kwa sababu zitakuwa na upungufu wa darasa moja.
Kila mwanafunzi hugawiwa Sh22,244 kila mwaka za kugharamia masomo.Isitoshe, shule kadhaa zitasalia na nafasi tupu zisizotumika hali inayosubiriwa kwa hamu kufuatia malalamishi kuhusu msongamano katika shule za sekondari tangu sera ya kusajili wanafunzi wote ilipoanzishwa 2014.
Hata hivyo, walimu wakuu wa shule za msingi sasa watasimamia mabilioni yaliyotengewa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari za msingi.
“Mambo yatabadilika sana hasa kibiashara. Kama fundi anayeunda masanduku ya shule, nimelazimika kubadilisha mbinu ya mapato kutokana na ukosefu wa biashara. Niliamua kujipanga mapema nikijua hakutakuwa tena na wanafunzi wa Kidato cha Kwanza, kwa hivyo ninaunda stovu badala yake,” anasema mfanyabiashara wa Kisumu, Richard Omollo.
Leave a Reply