Mabadiliko ya kitenzi ‘-w-’ katika semi (Sehemu ya Pili) – Taifa Leo


KATIKA sehemu ya kwanza ya makala haya, nilionesha kazi mbalimbali za viambishi katika neno ‘amekuwa’. Nilikusudia kuweka wazi matumizi mwafaka ya vitenzi vya silabi moja hasa {-w-} katika kauli tulizozinukuu awali.

Kauli ya kwanza ni ya mtangazaji wa runinga ambaye kutokana na taarifa fulani ya utapeli alitahadharisha: *‘Wakenya tunapaswa tukuwe macho’. Kauli ya pili ni ya mwandishi wa makala katika gazeti la Taifa Leo ambaye alipokuwa akitoa maoni kuhusu utendakazi wa jaji fulani alisema: ‘… hajakuwa akikubaliana kimahubiri na maombi ya EACC…’.  

Ili kuzitolea kauli hizo mbili hukumu mwafaka, itanibidi sasa nizungumzie dhima ya viambishi katika neno ‘tukuwe’ linalojitokeza katika kauli ya mtangazaji wa habari. Kiambishi {tu} kinawakilisha nafsi ya kwanza wingi. Kiambishi {ku} ambacho aghalabu hutoweka katika mazingira fulani ya kisarufi, ni kijalizo. Kiambishi {-w-} ni mzizi wa kitenzi husika ilhali {e) kinatekeleza dhima ya kuonya; katika muktadha huu.

Katika sehemu fulani ya makala haya, nimetaja mazingira ya kisarufi ambapo kijalizo {ku} cha vitenzi vya silabi moja hutoweka. Mojawapo ya mazingira hayo ni kinapotanguliwa na vitenzi visaidizi kama vile ‘pasa’ au ‘juzu’. Katika mazingira hayo, ambapo kiambishi cha nafsi hujitokeza katika kitenzi cha silabi moja, basi ni kosa kujumuisha kijalizo katika kitenzi hicho hicho. Mathalani, hapakuwa na haja mtangazaji tunayemrejelea kukijumuisha kijalizo baada ya kutumia kiambishi {tu} cha nafsi katika kitenzi (-w-).

[email protected]

…MAKALA YATAENDELEA



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*