CHAMA cha Madaktari wa Mifugo Kenya (KVA) kimeitaka serikali kusitisha kampeni ya chanjo ya mifugo hadi washikadau wote wakiwemo wataalamu wa mifugo, wakulima na viongozi ashirikishwe ipasavyo katika kupanga na kutekeleza zoezi hilo.
Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, KVA ilisema kuwa ingawa inaunga mkono kikamilifu juhudi za kudhibiti magonjwa ya mifugo kama vile miguu na midomo na Peste de Petis Ruminants kupitia kampeni endelevu, masuala kadhaa ya yanaathiri mafanikio ya mpango wa chanjo.
Kwa madaktari wa mifugo, mojawapo ya changamoto kubwa zinazokwamisha zoezi hilo ni ukosefu wa uaminifu unaokabili utawala wa Kenya Kwanza ambao hatua zao, walibainisha, zimeondoa “imani yoyote ambayo Wakenya walikuwa nayo na taasisi za serikali” na kufanya iwe vigumu kwao kuamini mipango ya serikali.
Pia waliikosoa serikali kwa kushindwa kutoa uhamasishaji wa kutosha kwa umma, jambo ambalo walisema limechochea upinzani mkubwa na upotoshaji miongoni mwa wafugaji na umma kwa ujumla.
Chama hicho pia kilibaini kuwa ugatuzi wa huduma za mifugo ulifanya changamoto za uratibu katika udhibiti wa magonjwa kuwa mbaya zaidi kwani kaunti zina idara duni za mifugo.
Pia, kuingiza siasa katika zoezi hilo la chanjo kumeathiri vibaya kampeni nzima, huku madaktari wa mifugo wakisema jambo hilo limewafanya wananchi kujitenga na lengo la kudhibiti magonjwa hatari ya mifugo na hivyo kuhatarisha zaidi mafanikio ya mpango huo.
Ni kwa sababu hizi ambapo KVA, kupitia kwa mwenyekiti wake wa kitaifa, Dkt Kelvin Osore, inataka Serikali kuahirisha mchakato wa chanjo ya mifugo hadi wakati Wakenya na wataalamu katika sekta hiyo watakuwa wamefahamishwa kikamilifu kuhusu zoezi zima.
“Serikali inafaa kusitisha zoezi la sasa ili kuruhusu muda wa kutosha wa uhamasishaji wa umma na kushughulikia maswala kutoka kwa Wakenya. Hii itasaidia kuhakikisha kuwa wafugaji wanaelewa manufaa ya chanjo na kushiriki kikamilifu katika mpango huo,” Dkt Osore alisema.
Kuharakisha mpango huu wakati ambapo Wakenya wengi hawako tayari kushiriki kutasababisha kutofaulu, chama hicho kilionya.
Madaktari hao wa mifugo pia wanataka serikali itambue hofu na wasiwasi ulioibuliwa na Wakenya kuhusiana na zoezi hilo na kuwapa taarifa zitakazowasaidia kufanya maamuzi sahihi kuhusu iwapo wanyama wao watachanjwa au la.
Chama kinaitaka serikali kuzindua kampeni dhabiti ya kuelimisha wakulima kuhusu zoezi hili na kujibu maswali yote yanayoulizwa na wananchi.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA
Leave a Reply