Madaktari wabadilisha tiba ya Papa Francis kukabiliana na ‘hali tata’ – Taifa Leo


VATICAN CITY, VATICAN

MADAKTARI wamebadilisha aina ya matibabu wanayompa kiongozi wa kanisa Katoliki ulimwenguni Papa Francis aliyepatwa maambukizi ya mfumo wa kupitisha hewa ili kukabiliana na ‘hali changamano iliyoibuka’ na atasalia hospitalini kwa muda mrefu uwezekanavyo, Vatican ilisema Jumatatu.

“Matokeo ya vipimo vilivyofanywa katika siku za hivi karibuni na leo vimeonyesha maambukizi fulani ya mfumo wa kupitisha hewa, hali ambayo imelazimu abadilishiwe matibabu,” ikasema taarifa fupi.

“Vipimo vyote vilivyofanywa leo (Jumatatu) vimeonyesha taswira ya hali changamano itakayohitaji kwamba aendelee kusalia hospitalini,” taarifa hiyo ikaongeza.

Papa Francis mwenye umri wa miaka 88, amekuwa akitatizwa na maambukizi katika chemba ya kutoa hewa kwa zaidi ya juma moja na alilazwa katika Hospitali ya Gemelli jiijini Rome Ijumaa wiki jana.

Msemaji wa Vatican Matteo Bruni alisema Jumatatu kuwa kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki ulimwenguni “alikuwa mchangamfu”.

Hakufafanua ikiwa Papa huyo alikuwa akiugua maambukizi ya bakteria au virusi lakini akasema maelezo zaidi kuhusu hali ya kiongozi huyo ingetolewa jana jioni.

Ingawa maambukizi ya bakteria yanayoweza kutibiwa kwa dawa aina ya “antibiotics”, maambukizi ya virusi hayawezi.

Virusi husalia mwilini kwa muda mrefu, lakini  mgonjwa anaweza kusaidiwa kwa kupewa dawa ya kupunguza makali yao au kusaidia mwili kupambana na maambukizi.

Jumatatu, Februari 17, 2025, Vatican ilisema kuwa kuwa mpango wa Papa kuhutubia umma kila wiki ulioratibiwa kufanyika Jumatano katika uwanja wa St Peter Square ulifutiliwa mbali, kutokana na “kulazwa kwa Baba Mtakatifu.”

Awali, madaktari wa Papa Francis, waliamuru kwamba afanyiwe vipimo jumuishi, hali iliyomfanya Francis kuongoza misa ya kila wiki Jumapili katika St Peters Square. Aidha, hakuweza kuongoza misa maalum ya wasanii kuadhimisha Mwaka Maalum wa Kanisa Katoliki.

Papa Francis, ambaye ni raia a Argentina, amehudumu kwa karibu miaka 12 kama kiongozi wa Kanisa Katoliki.

Mnamo Machi 2023 Papa alilazwa kwa siku tatu katika Hospitali ya Gemelli baada ya kuugua maradhi ya “bronchitis”.

Mnamo Desemba mwaka huo huo, alilazimika kufutilia mbali ziara yake nchini Muungano wa Milki za Kiarabu kuhudhuria Kongamano la Kimataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) baada ya kupata na aina nyingine ya maradhi.

Papa Francis amekumbwa na changamoto za kiafya maishani mwake, kiasi kwamba akiwa na umri wa miaka 21 moja kati ya mapafu yake iliondolewa.

Waumini waliotembelea Vaticana jana walielezea matumaini yao kwamba Francis atapata afueni hivi karibuni.

“Bila shaka tunamtakia afueni ya haraka,” akasema Kasisi Tyler Carter, kasisi wa Kanisa Katoliki nchini Amerika.

“Yeye ni baba yetu na mchungaji wetu. Kwa hivyo, tunataka aendelee kuwa buheri wa afya ili atubariki,” akaongeza.

Naye Manuel Rossi, mtalii kutoka Milan, Italia, alielezea kuingiwa na mshtuko Papa Francis alipokosa kujitokeza kuongoza misa Jumapili.

“Niko na umri wa miaka 18 na hivyo nimewaona Mapapa wachache zaidi maishani mwangu. Hii ndio maana nimekuwa karibu naye. Namtakia afueni ya haraka,” akaeleza.

IMETAFSIRIWA NA CHARLES WASONGA



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*