Maendeleo ya biashara za vyuma vikuukuu kupitia sheria mpya – Taifa Leo


BARAZA la vyuma vikuukuu linatarajia kupigwa jeki katika vita dhidi ya uharibifu wa miundomsingi ya umma.

Wanaoharibu miundomsingi, kwa mfano ile ya barabara, hulenga kuendeleza biashara za vyuma vilivyotumika.

Hii ni kulingana na mwenyekiti wa baraza hilo Francis Mugo anayeamini Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Biashara 2024 utawasaidia kushirikiana na Wizara ya Usalama kukabili uharibifu.

Mswada huu unalenga kubadilisha sehemu ya 4 ya Sheria ya Vyuma Vikuukuu na kuimarisha mfumo wa uongozi wa baraza hilo.

“Mapendekezo ya marekebisho ya sheria yatajumuisha wizara ya usalama katika baraza na kutakuwa na ushirikiano wa karibu kazini kwa uwepo wa maafisa wa polisi,” akasema Bw Mugo.

Bw Mugo alisema haya alipzungumza na vyombo vya habari kuhusu mafanikio yao katika mwaka mmoja.

Mwenyekiti huyu anaripoti kuwa bado kuna visa vya wizi wa vyuma kutoka makazi ya watu na na barabarani.

Kulingana na Bw Mugo, tangu aingie afisini Februari 2023, kumekuwa na ufanisi wa kupigiwa mfano katika sekta hii.

“Tangu nichukue hatamu za uongozi, tumefaulu kukabili wizi na kuhakikisha kuna vyuma vya kutosha kuendeleza uzalishaji wa vyuma na kuimarisha mazao ya sekta hii,” akasema Bw Mugo.

Baraza hili limesema juhudi zake zimesaidia kutunza ajira za humu nchini, kustawisha viwanda na kuinua uchumi.

“Tumejenga msingi wa sekta endelevu kwa hivyo tumewainua washikadau muhimu. Sasa, wanabiashara wa vyuma vikuukuu, wanaouza nje ya nchi, na wayeyushaji wa vyuma  wanafanya kazi katika mfumo wazi wa kisheria,” Bw Mugo alisisitiza.

Aliteuliwa kukabili visa vya uharibifu wa miundomsingi ya umma baada ya kukithiri kwa uharibifu.

Marufuku ya uuzaji nje wa vyuma na biashara hii iliyotangazwa na Bw Kenyatta Januari 2022, ilipingwa vikali na baadhi ya Wakenya wakidai sekta hii imeajiri vijana wengi.

Rais William Ruto, aliyekuwa Naibu Rais wakati huo, alipinga hatua hiyo akisema ni mikakati ambayo ililenga kulemaza kiuchumi wananchi wenye mapato ya chini.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*