MAMIA ya wakazi wamehama makazi yao kufuatia mvua kubwa iliyofanya mto Nyando, kaunti ya Kisumu kuvunja kingo zake.
Mvua hiyo ilisababisha mafuriko katika barabara kuu ya Kisumu-Nairobi kwenye daraja la Ahero, na kusababisha nyumba, biashara, mashamba na miundombinu muhimu kujaa maji, na kuziacha familia zilizoathiriwa zikihitaji msaada wa haraka wa kibinadamu.
Hofu ilitanda katika mji wa Ahero huku maji yaliyokuwa yakiongezeka yakilazimisha wakazi kuhama kutafuta hifadhi kando ya barabara na mali zao baada ya nyumba zao kusombwa na maji ya mafuriko.
Biashara pia zilipata hasara kubwa huku Shule ya Wasichana ya Ahero ikifunikwa kabisa baada ya River Nyando kuvunja kingo zake. Mafuriko hayo yalisababisha usumbufu mkubwa huku wakazi wakielezea wasiwasi wao kuwa mvua itazidisha hali ikiendelea kunyesha.
Mark Ochieng, alisema mafuriko hayo ni ya pili kutokea katika siku za hivi majuzi na akatoa wito kwa serikali ya kitaifa na kaunti kutoa suluhu la kudumu.
Chifu wa Kakola Ombaka Neto Awich alisema angalau familia 78 zimehamishwa katika eneo la Kakola linalokabiliwa na mafuriko.Kufikia Jumamosi asubuhi, ekari 200 za ardhi zilikuwa zimesombwa na maji’Watu waliokimbia makazi kwa sasa wanatafuta hifadhi katika nyumba za majirani na jamaa zao katika nyanda za juu,’ alisema Bw Awich.
Meneja wa Jiji Abala Wanga alisema hatua za haraka zilichukuliwa kusaidia wakazi wa Kapuothe na Alewra baada ya Mto Nyamasaria kuvunja ukingo wake.
Alitoa wito kwa wakazi walioathirika kuhamia kambi ya muda iliyowekwa katika Shule ya Msingi ya St Vitalis Nanga.Bw Wanga alisema kuwa kuhamishwa kwao kutaruhusu kaunti kuchukua hatua muhimu kukabiliana mafuriko.Haya yalijiri huku mamia ya familia katika kijiji cha Kapuothe, Nyalenda, wakikabiliana na athari za mafuriko makubwa ambayo yamewafanya kutoroka makazi yao.
‘Tunataka suluhu la kudumu,’ alisema Steve Omondi, mkazi. ‘Hii hutokea kila mwaka, lakini serikali inachukua hatua tu baada ya mvua kuanza. Inahitaji kushughulikia suala hili kabla ya mafuriko kurejea tena.”Alieleza kuwa Mto Nyamasaria ndicho chanzo kikuu cha mafuriko na kutoa wito kwa mamlaka kuelekeza maji ya mto huo katika Ziwa Victoria.
Leave a Reply