Mahakama ilivyompa afueni Gavana Mwangaza baada ya kutimuliwa ofisini – Taifa Leo


IKIWA kuna mtu ambaye 2024 alifurahia maamuzi ya mahakama, ni Gavana wa Meru Kawira Mwangaza.

Kwa sasa, Gavana huyo anahudumu katika wadhifa huo kwa muda wa siku 120 (miezi mitatu) kuanzia Desemba 18, 2024 kwa agizo la mahakama kusubiri kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi yake kupinga kutimuliwa kwake na Seneti.

Gavana Mwangaza, sasa amejifunga kibwebwe kutetea kiti alichokinyakua katika ushindani mkali dhidi ya Bw Mithika Linturi (wa chama cha UDA) na gavana wa zamani Bw Kiraitu Murungi.

Mwangaza aliwabwaga miamba wa siasa na kutwaa ushindi kama mwaniaji huru kwa kuzoa kura 209,148, Bw Linturi alijizolea kura 183,859 naye Bw Murungi alinyakua nafasi ya tatu kwa kupata kura 110,814.

Tangu Bi Mwangaza atwae ushindi huo, hajatulia huku akipigwa vita na madiwani (MCA).

Mawakili Elias Mutuma, Prof Elisha Ongoya na Milton Mugambi Imanyara wanaomwakilisha gavana huyo walieleza mahakama kwamba watafanya kila juhudi kutetea mwanasiasa huyo ambaye ameonyeshwa cha mtema kuni na wapinzani wake.

Bw Imanyara alisema ijapokuwa Bi Mwangaza amekumbwa na upinzani mkali, “vita vya kupinga uongozi wake havitafua dafu. Huyu ndiye wakazi wa Meru walimchagua kuwa Gavana wao na inafaa apewe muda akamilishe muhula wake wa uongozi.”

Bunge la Seneti liliidhinisha uamuzi wa bunge la kaunti ya Meru na kumtimua uongozini Bi Kawira Mwangaza mnamo Agosti 21, 2024.

Maseneta 26 walipinga kura kuunga mkono mashtaka matatu dhidi ya Bi Mwangaza.

Lakini Bi Mwangaza aliwasilisha kesi kortini kabla ya Gazeti Rasmi la Serikali kuchapisha uamuzi wa kumwondoa mamlakani.

Hata hivyo, Seneti iliwasilisha ombi la kufutiliwa mbali agizo la kusitisha uamuzi wa kumwondoa afisini gavana huyo.

Seneti ilimkosoa Bi Mwangaza kwa kumshtaki Spika wa Bunge hilo Amason Kingi, badala ya kushtaki bunge lenyewe.

Jaji Bryan Mwamuye alikubalia ombi la kushirikisha bunge la kaunti ya Meru kushiriki katika kesi hiyo na vilevile Bi Zipora Kinya aliyewasilisha hoja ya kumtimua afisini Gavana Mwangaza, lakini akaongeza muda wa mwanasiasa huyo kuhudumu kwa siku 120 akisema itakuwa hasara kwake akiondolewa kabla ya kesi kuamuliwa.

 



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*