Mahakama yaidhinisha Sh1.3bn kama fidia kwa wakazi wa Owino Uhuru – Taifa Leo


ZAIDI ya waathiriwa 3,000 wa sumu ya chuma cha risasi katika kijiji cha Owino Uhuru, Mombasa, wamepata ushindi mkubwa baada ya Mahakama ya Juu kuthibitisha uamuzi ulioagiza kuwa serikali iwafidie Sh1.3 bilioni kwa kupoteza maisha au kupata madhara ya kiafya zaidi ya miaka 10 iliyopita.

Majaji wa Mahakama ya Juu Mohamed Ibrahim, Smokin Wanjala, Njoki Ndung’u, William Ouko na Isack Lenaola waliamua kwamba Mahakama ya Rufaa ilifanya uamuzi usio sahihi kwamba watu waliopata majeraha ya kiafya katika mtaa huo hawakutambulika.

“Ili kuepusha shaka tunathibitisha Sh1.3 bilioni zilizotolewa na Mahakama Kuu kama fidia ya jumla ya kupoteza maisha na majeraha ya kibinafsi. Kiasi hicho sio tu kwa manufaa ya watu 11 waliokata rufaa bali ni kwa familia 450 na wakazi wa kijiji cha Owino Uhuru ambacho kinajumuisha takriban ekari 13.5,” majaji walisema katika uamuzi uliotolewa jana.

Walisema kuwa Mahakama ya Mazingira na Ardhi (KKKT) iliyotoa fidia hiyo ilifikia kiwango sahihi cha fidia ya majeraha ya kibinafsi na vifo na kwamba kiasi hicho hakikuwa kikubwa sana wala mahakama haikuzingatia jambo lisilohusika.

Pia, majaji walisema kulikuwa na ushahidi wa athari za moja kwa moja za kiafya na vifo kwa wakazi kama ilivyoonyeshwa kutoka kwa ripoti za matibabu zilizowasilishwa mbele ya mahakama.

“Halikuwa tukio la mara moja bali ni ukiukaji wa mara kwa mara ambao uliendelea kwa zaidi ya miaka saba wakati kiwanda cha kusafisha chuma kilikuwa kikifanya kazi na baadaye,” walisema majaji.

Majaji hao pia walisema kuwa walalamishi, ambao ni pamoja na Phyllis Omido waliwasilisha ushahidi na kuthibitisha kwa kuridhisha katika mahakama ya ELC kwamba kijiji cha Owino-Uhuru kilikuwa na watu 3000 katika familia 450.

Rekodi ya ELC inaonyesha kwamba angalau watu 20 walikufa kwa sababu ya kuwa na risasi.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*