Mahitaji ya unga Krismasi ikikaribia yafanya bei ya mahindi kuongezeka na wakulima kutabasamu – Taifa Leo


WAKULIMA wa mahindi sasa wanavuna pakubwa kufuatia ushindani wa bei kati ya Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) na kampuni za kusaga unga huku mahitaji ya bidhaa hiyo yakiongezeka.

Hii inajiri huku bei za soko zikipanda licha ya mavuno mengi msimu huu.

Ushindani kati ya NCPB na kampuni  umefanya bei ya bidhaa hiyo kupanda hadi Sh4,000 kwa gunia la Kilo 90 kutoka Sh2,600 mwezi uliopita na kuwanusuru wakulima ambao kwa miaka miwili iliyopita wamekuwa wakipata hasara kutokana na bei ya chini.

Huku NCPB ikilenga kununua hadi magunia milioni moja kwa Sh3,500 kwa gunia la Kilo 90,  kampuni za kusaga unga  na wafanyabiashara wengine wamepandisha bei kutoka Sh2,600 hadi Sh3,850 ili kuwavutia wakulima.

Nchi ina mavuno mengi ya mahindi msimu huu kufuatia usambazaji wa mbolea ya ruzuku ya serikali na mazao mengi ya muda mfupi kutokana na mvua za El Nino.

“Tunatazamia mavuno mengi ikilinganishwa na msimu uliopita ambapo tulipata magunia kati ya milioni 40 na 60 lakini takriban magunia milioni 75 ya kilo 90 yatapatikana msimu huu,” Waziri wa Kilimo Andrew Karanja alisema wakati akitetea bei iliyowekwa ya mahindi akisema kuwa itasaidia kudumisha bei za Unga kwa bei ya sasa ya Sh130 kwa kila pakiti ya Kilo mbili.

Kaunti ya Trans Nzoia inatazamiwa kupata takriban magunia milioni 5.3 ya mahindi  huku takriban milioni 3.3 yakiuzwa sokoni.

Kaunti ya Uasin Gishu, eneo lingine la kuzalisha mahindi linatarajiwa kuvuna takriban magunia milioni 4.5 ya mahindi msimu huu ambapo zaidi ya magunia milioni 2.5 yatauzwa sokoni.

“Ushindani kama huu wa kampuni za kusanga unga na NCPB ambao umefanya bei kupanda utawafanya wakulima wengi kuwekeza katika kilimo hiki msimu unaofuata na kupata faida nzuri,” alisema James Kemboi kutoka Moiben, Kaunti ya Uasin Gishu.

NCPB kufikia sasa imenunua takriban magunia 10,000 ya mahindi kutoka North Rift huku wakulima wengi wakihifadhi zao hilo kwa kutarajia bei nzuri zaidi.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*