ALIYEKUWA kiongozi wa Mungiki Maina Njenga na mamia ya wafuasi wake Jumamosi walivamia mkutano wa maombi ya madhehebu mbalimbali katika Kaunti ya Nyeri ambapo aliyekuwa Naibu wa rais Rigathi Gachagua alitarajiwa kuongoza.
Katika zogo lililofuata, Bi Rigathi alikuwa aliondolewa kwa haraka na walinzi wake kutoka uwanja wa Kamukunji katika mji wa Nyeri.
Hali ya wasiwasi na hali ya suitafahamu ilitawala Bw Njenga na wafuasi wake waliokuwa katika msafara wa magari kadhaa walipovamia uwanja huo mwishoni mwa sherehe wakiimba ‘Ndovu! Ndovu’ huku Bw Njenga akiwa juu ya paa la gari lake la Toyota Prado chini ya ulinzi mkali.
Jambo hili linaonekana kuwashangaza waandalizi wa hafla hiyo, huku mhubiri mmoja anayeishi Nairobi maarufu kama Padri Maina wa OTC akikatiza maombi yake ya mwisho na kurejea kwenye kiti chake mkanyagano ukizuka huku mamia ya waumini wakikimbilia usalama katika njia tofauti.
Ilikuwa ni wakati huu ambapo mchungaji Dorcas aliondolewa kwa haraka kupitia mlango wa nyuma akiandamana na viongozi wengine kadhaa wa kanisa.
Katika hali hiyo, maafisa wachache wa polisi waliokuwa katika uwanja huo pia waliondoka ukumbini huku afisa mmoja wa kike alisikika akisema ‘tuondoke Maina Njenga amekuja”.
Hata hivyo, baada ya ibada kutatizwa kwa muda mfupi Bw Njenga alikaribishwa katika jukwaa kuu ambapo alijiunga na makasisi walioonekana kutikiswa na mabadiliko hayo.
Kulingana na ratiba ya siku hiyo iliyoonwa na Taifa Jumapili, Bw Gachagua aliorodheshwa kuwa mmoja wa wazungumzaji wakuu katika mkutano ulioandaliwa hasa na makanisa ya kiinjililisti kuombea taifa.
Inagawa hivyo, Bw Gachagua hakufika kama ilivyotarajiwa huku mke wake akitoa salamu lakini hakueleza sababu ya kutokuwepo kwake.Vyanzo huru vilifichua kuwa Bw Gachagua alikuwa katika hoteli moja katika mji wa Nyeri lakini akakosa kuhudhuria mkutano huo zilipoenea habari kwamba Bw Njenga alikuwa mjini.
Hali ya utulivu iliporejea Kasisi Maina alikaribishwa na kumwalika Bw Njenga kuhutubia mkutano ambapo hakuonekana kama aliyevamia mkutano kwa nia ya kumpinga Bw Gachagua.’Sikuja hapa kwa sababu ya siasa au mtu yeyote, kwa vyovyote vile mimi ni askofu, nilisikia kuna mkutano wa maombi na niliamua kuungana nanyi,’ alisema huku vijana wake wakiimba ‘Ndovu! Ndovu!”
Wakati huo huo, Njenga alionekana kumshutumu Mungiki, kundi ambalo aliongoza zamani akisema ‘wavulana’ wake wametajwa kwa nia mbaya kwa majina ‘ya kizamani’ ya 1990.
Aliongoza kundi la vijana walioandamana naye katika kutubu dhambi za siku zilizopita.Walipiga magoti mbele ya makasisi ambapo waliapa kusahau maisha yao ya nyuma na kuomba msamaha.
“Kuanzia sasa, kwenda mbele sitamtukana mtu yeyote, nitajiunga na makanisa mengine ambayo yatakuwa yakiombea taifa hili, tunahitaji maombi mengi, hata hivyo hayapaswi kuwa katika eneo la Mlima Kenya pekee, yapanuliwe katika maeneo mengine ya nchi,” alisema.
Bw Njenga hata hivyo, alijiepusha na siasa licha ya wito wake wa hivi majuzi kwa wakazi wa eneo la Mlima Kenya kumuunga mkono rais William Ruto.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA
Leave a Reply