MWISHONI mwa miaka ya 1990 na mwanzoni mwa miaka ya 2000, kutajwa tu kwa neno “Mungiki” kulifanya wakazi wengi wa eneo la Mlima Kenya na sehemu za Nairobi kutetemeka.
Kundi hilo lilihusishwa na Bw Maina Njenga, kiongozi wake wakati huo lakini ambaye baadaye alitangaza kuokoka na kiongozi wa Wakfu wa Amani Sasa Foundation.
Bw Njenga kwa miaka mingi pia amejitosa katika siasa – wakati mwingine kama mgombeaji, wakati mwingine akichukuliwa kuwa ‘mfalme’ lakini mara nyingi akiasi. Mnamo Desemba 31, 2024, Bw Njenga alitangaza tena nia yake ya kujitosa katika siasa za Mlima Kenya kwa lengo la kuzima ushawishi wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua katika eneo hilo na kuunga mkono Rais William Ruto.
Hatua hiyo imeibua sintofahamu ikizingatiwa kuwa katika maandalizi ya uchaguzi wa 2022, Bw Njenga alikuwa mkosoaji mkubwa wa Dkt Ruto na kumuunga mkono mgombeaji urais wa Azimio Raila Odinga.
Hatimaye Rais Ruto alipata kura za Mlima Kenya huku timu inayoongozwa na mgombea mwenza Rigathi Gachagua ikishinda ujanja wa Bw Njenga na vinara wengine wa Azimio kutoka eneo hilo.
Tukio la hivi majuzi kaunti ya Nyeri ambalo lilijiri wakati ambapo Rais Ruto na utawala wake wa Kenya Kwanza wanaonekana kutatizika kupata uungwaji mkono katika eneo la Mlima Kenya baada ya kutofautiana na Bw Gachagua, sasa limeibua maswali kuhusu mpango wa Bw Njenga na iwapo yeye ni jibwa la vita vya kisiasa, au anajiwakilisha binafsi. Pia, kuna hofu kwamba shughuli zake mpya zinaweza kuibua upya magenge kama Mungiki kwa sura tofauti.
“Mungiki,” neno la Kikuyu linalotokana na neno “Muingi,” ambalo linamaanisha “umati”, liliibuka kama vuguvugu la kidini, likitoa msukumo kutoka kwa tamaduni na desturi za jadi za Wakikuyu.
Madhumuni ya kundi hilo lilikuwa kuunganisha na kuhamasisha raia wa eneo la Kati la Kenya kupigana na kile walichochukulia kama utumwa wa kiakili, ambao washiriki wake walidai uliathiriwa na Ukristo.
Lakini baada ya muda, likawa biashara ya uhalifu ya kidini ambayo shughuli zake zilijumuisha unyang’anyi, vitisho na utapeli wa kisiasa. Kuanzia enzi ya Daniel Moi, Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta, shughuli za kundi hilo kila mara zimekuwa zikizua mgawanyiko mkubwa kimaoni.
Jambo muhimu zaidi, magenge ya Mungiki pia yalitumiwa katika mashambulizi ya kulipiza kisasi au kama “watetezi” wa jamii wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007/2008.
Genge hilo hatimaye liliharamishwa katika muhula wa pili wa utawala wa Kibaki – huku Waziri wa Usalama wa Ndani wa wakati huo John Michuki akiwa mstari wa mbele – na vita dhidi ya kundi hilo zililiangamiza baada ya mauaji ya kiholela na kukamatwa kwa wanachama wengi.
Hata hivyo, hata baada ya kupigwa marufuku na kuzimwa na nguvu za serikali, kundi hilo linafikiriwa kuwa lilienda chini ya maji na mara nyingi limetumika kwa siri. Hata hivyo, Bw Njenga – ambaye kwa miaka mingi amekuwa akipambana na kukamatwa, kesi mahakamani na hata madai ya majaribio ya mauaji – alibadilisha jina kuwa mhubiri -mwanasiasa.
Wakati wa enzi za Mungiki, Bw Njenga alishirikiana na binamu yake Ndura Waruinge lakini baadaye wakaachana. Bw Waruinge alisema alisikia “sauti kutoka kwa Mungu” ambayo ilimfanya aachane na kikundi hicho na kujiunga na Ukristo.
Bw Waruinge, ambaye sasa ni mhubiri, ni kiongozi wa kiroho wa kanisa la Synagogue Arena of Liberty Church.
Bw Njenga tangu wakati huo amekashifu Mungiki na kutupilia mbali uvumi kwamba Amani Sasa Foundation ina uhusiano na dhehebu hilo lililoharamishwa. Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2022, Bw Njenga alisema yeye ni kiongozi wa chama na alifaa kutambuliwa kama kinara mwenza wa Azimio.
“Tunaposonga mbele, sitaki nitambuliwe kama kiongozi wa zamani wa Mungiki, mimi ni kinara mwenza wa Azimio,” alisema.
Kwa nyakati tofauti, amejitambua kama mfalme wa Mlima Kenya na kutanua misuli kwa kufanya mikutano inayohudhuriwa na mamia ya vijana. Jaribio lake la kushinda kiti katika uchaguzi, hata hivyo, limekuwa likiporomoka kwa miaka mingi.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA
Leave a Reply