Majangili waua afisa wa magereza, waachilia mahabusu wanane hatari – Taifa Leo


MAAFISA  wa usalama kutoka kwa Kitengo cha Kupambana na fujo (GSU) na Jeshi la Ulinzi la Kenya katika Kaunti ya Samburu, wanawasaka majangili waliompiga risasi na kumuua afisa wa magereza kabla ya kusaidia wafungwa wanane kutoroka.

Afisa  huyo wa magereza aliuawa kwa kupigwa risasi  na wafungwa wanane wakatoroka wakati wa kisa hicho cha Jumanne asubuhi, baada ya majangili waliokuwa na silaha kuvizia gari la polisi lililokuwa likisafirisha washukiwa hadi mahakama ya kuhamishwa huko Baragoi.

Shambulizi hilo lilitokea katika eneo la Charda kwenye barabara ya Maralal-Baragoi.

Kamanda wa polisi kaunti ya Samburu Thomas Ototo alithibitisha kisa hicho na kusema kuwa majangili walilenga gari hilo, kwa nia ya kuwaachilia wafungwa.

“Washukiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya makosa mbalimbali ya jinai, ikiwa ni pamoja na kumiliki bunduki kinyume cha sheria, mauaji, wizi wa kutumia nguvu na unajisi,” alieleza Ototo.

Majangili waliokuwa na silaha kali walifanikiwa kuwazidi nguvu maafisa wa usalama  na  kuwezesha washukiwa wote wanane kutoroka

“Tumeanzisha operesheni ya pamoja ya usalama, inayojumuisha maafisa wa Polisi wa Kenya na Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), Kitengo cha polisi wa kupambana na fujo (GSU) na maafisa wengine wa kawaida wa polisi katika harakati za kuwasaka washukiwa waliotoroka na kuwatia nguvuni washambuliaji,” alisema kamanda wa polisi.

Vikosi vya usalama vinafanya masako  Charda, Mbukoi, na Marti eneo la  Samburu Kaskazini,  ambalo linakabaliwa na tisho la kutumbukia tena katika uhalifu uliopangwa.

“Kufikia sasa tumewakamata tena washukiwa wawili. Hatutalegea katika harakati zetu za kuwasaka washukiwa wengine waliotoroka na hata waliohusika na kitendo hiki kiovu. Watakabiliwa na mkono wa sheria,” Bw Ototo aliambia Taifa Leo jana.

Mahabusu waliotoroka wametambuliwa kama Kennedy Lekisaat (mshukiwa wa unajisi), Ewoi Lonyogorot (aliyeshtakiwa kwa unajisi), Namulem Losam (anayekabiliwa na mashtaka  ya kupatikana na bunduki), Lorunyei Akware (anayeshitakiwa kwa kosa la unajisi).

Wengine ni Lopasho Ekoriana (unajisi), Saul Lekisaat (unajisi), Lokwawi Adoro (mauaji/wizi wa kutumia nguvu) na Golong Arii (kushambulia)

Wakaazi wa eneo hilo wameelezea hofu yao kutokana na ongezeko la visa vya ujangili katika barabara ya Maralal-Baragoi, wakitaka maafisa wa usalama waimairishwe  doria.

Mkuu huyo wa polisi pia aliwataka wananchi kutoa taarifa zozote zinazoweza kusaidia kukamatwa tena kwa waliotoroka na washambuliaji



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*