Majonzi ya familia Kisii binti yao mwanachuo kuporomokewa na choo akiwa msalani – Taifa Leo


KATIKA miaka yake ya ujana, Celine Nyangweso, 23, alikuwa mwingi wa ndoto na tumaini la pekee kwa familia yake.

Lakini kifo cha mwanafunzi huyo wa mwaka wa mwisho katika chuo anuwai cha kitaifa cha Kisii, kimeacha familia yake ikiwa katika uchungu wa kufifisha ndoto zao.

Celine alifariki siku ya Ijumaa, Januari 31, 2025 baada ya kutumbukia kwenye choo, katika mtaa wa Mwembe, viungani mwa mji wa Kisii alikokuwa akiishi na mpenziwe.

Sakafu ya choo hiyo iliporomoka, alipokuwa ndani kwa haja nyakati za usiku.

Wawili hao walikuwa wametayarisha na kula chakula cha jioni pamoja. Walipojiandaa kwenda kulala, Celine alihisi anahitaji kuitikia wito wa kuenda msalani.

Kwa kuwa vyoo vya ploti yao vilikuwa umbali wa mita chache kutoka chumba chao, alimwomba mpenzi wake amsindikize ili ajihisi salama atakapokuwa msalani.

Ghafla alipokuwa akimngoja nje ya choo hicho, mpenzi huyo alimsikia Celine akipiga kelele ya kuomba msaada. Sakafu ya choo hicho ilikuwa imeporomoka pindi tu alipoufunga mlango wake, alikuwa anamezwa ndani ya uchafu upatikanao humo.

Akidhamiria kumwokoa, mpenzi huyo alijaribu kuingia kwenye choo hicho kilichoporomoka lakini juhudi zake zote zilikatizwa na uvundo mwingi uliokuwa ukitoka mle.

Hata majirani waliokuwa wamejitokeza kwa wingi baada ya kusikia purukushani hizo walishindwa kwani juhudi zao za kumvuta nje ziligonga mwamba.

Kikosi cha kaunti cha kukabiliana na majanga ya dharura kilipowasili na polisi, waliuondoa uchafu wote uliokuwemo mle lakini Celine alikuwa amekata roho.

Mwili wake ulichukuliwa na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kisii (Ktrh) huku marafiki na jamaa waliokuwa wamefahamishwa kuhusu tukio hilo wakitokwa na machozi.

Taifa Leo ilipotembelea familia ya Celine nyumbani kwao Kenyenya, eneobunge la Bomachoge Borabu, kulikuwa na shughuli nyingi huku waombolezaji waliofika kufariji wazazi wake wakiingia na kutoka.

Mamake Celine, Everline Nyaboke alisimulia uchungu wa kufiwa na mtoto wake wa kwanza, ambaye alisema alikuwa amalize masomo yake mwezi ujao.

Babake Celine hakuwa nyumbani. Pamoja na jamaa wengine, alikuwa ameenda mjini Kisii kwa shughuli ya upasuaji wa maiti ya mwanawe.

Bi Nyaboke, mama wa watoto watano alisema kifo kilikuwa kimeipokonya familia yake tumaini lao la pekee. Alisimulia jinsi ilivyokuwa vigumu kwao kumsomesha binti huyo hadi elimu ya ngazi hiyo ya juu wakitumai kuwa atakuja kuwainua maishani.

“Tumekuwa tukifanya kazi za sulubu na mume katika mashamba ya watu ili kupata karo yake. Hata vyama vingi vya akiba vinatudai kwa kukopa hela zao kwa faida ya kumsomesha kifunguamimba wetu na wenzake wanne. Sasa hatujui tutakimbilia wapi. Hatujafahamu ni kwa nini Mungu ameamua kutuacha?” Bi Nyaboke alisema huku akibubujikwa na machozi.

Nyanya ya Celine-Teresia Abunga alikumbuka jinsi mjukuu wake alikuwa amemwalika kuhudhuria sherehe ya kufuzu kwake mjini Kisii ili waweze kusherehekea mafanikio yake lakini akajuta kwamba hilo halitafanyika.

“Alikuwa amenialika kwa sherehe yake ya kufuzu masomoni mwezi ujao.Nilikuwa nimemwahidi kuwa nitahudhuria sherehe yake ili nimpongeze kwa bidii yake. Tulikuwa na matumaini makubwa kwake kwamba ndiye ambaye angetuinua kutoka kwa umaskini uliokithiri kwetu,” Bi Teresia alisema kwa huzuni mwingi.

Kufuatia tukio hilo la kusikitisha, Wakenya wengi walijitokeza kwa wingi kuwahurumia familia iliyofiwa na wakati huo huo kunyooshea kidole cha lawama mamlaka kwa kile walichodai kuwa ni kutoweka jitihada za kutosha katika kuhakikisha ujenzi wa nyumba za kupangisha na huduma nyingine unatimiza viwango.

“Inasikitisha sana kwamba katika siku hizi bado tunarekodi visa vya watu kuanguka na kufa kwenye vyoo vya shimo ndani ya mji ambao viongozi wake wanajigamba kuwa mji huo umefikisha viwango vya kuwa jiji. Manispaa ya Mji wa Kisii inapaswa kuwaeleza wananchi kwa nini vyumba vilivyoko Mwembe, mita 500 kutoka katikati  mwa mji wa Kisii, viliachwa kufanya kazi na vyoo vya kuning’inia, visivyo vya kiwango. Mmiliki wa vyumba hivyo pia anapaswa kukabiliana na nguvu kamili za sheria,” Bw Mainga alisema.

Bi Linet Nyaboke, mama mwenye nyumba ambazo vyoo vyake viligharimu maisha ya Celine hata hivyo amejitetea dhidi ya madai kwamba ujenzi wa vyoo hivyo haukuwa wa viwango vinavyohitajika.

“Wapangaji wangu hawakuwa wameripoti kwangu iwapo walikuwa wameshuhudia dalili zozote za choo kuporomoka. Ninahusisha kuanguka kwavyo na mvua kubwa ambayo imekuwa ikinyesha,” landiledi huyo alisema.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*