SHUGHULI ya kuharibu shehena ya magunia 546 ya mchele mbovu wenye thamani ya Sh1.5 milioni iligeuka ghasia afisa wa polisi akijeruhiwa huku maafisa wengine wakitorokea usalama wao.
Maafisa wa serikali akiwemi Kamishna wa Kaunti ya Uasin Gishu Eddyson Nyale na Mkurugenzi Mkuu wa shirika la kukadiria ubora wa bidhaa (KEBS) Esther Ngari walikuwa katika zoezi la kuharibu mchele huo ulio na sumu ya aflatoxin.
Lakini machafuko yalianza katika eneo la kutupa taka la Huruma jijini Eldoret mnamo Alhamisi alasiri huku walala hoi wakipinga hatua ya kuharibu ‘chakula’ licha ya kuambiwa kuwa mchele huo ulikuwa na sumu.
“Ni mwiko kuharibu chakula hata ikiwa hakifai kwa matumizi ya binadamu tupeni tutakula na hatutakufa,” walipiga kelele wakielekea mahali mchele huo ulikuwa unaharibiwa.
Juhudi za viongozi hao kushawishi familia za kurandaranda mtaani zilizokasirika kuwa mchele huo haufai kwa matumizi ya binadamu, hazikufua dafu kwa sababu walianza kuwarushia askari mawe na vipande vya chupa kabla ya shughuli hiyo kutibuka.
Tulilazimika kusitisha azma yetu ya kuharibu mchele husika baada ya kile kilichotokea. Wahusika wa shambulio hilo hivi karibuni watakabiliwa na sheria
Maafisa wachache wa polisi waliokuwa wakilinda eneo hilo walizidiwa nguvu pale afisa mmoja wa polisi wa kike alipojeruhiwa vibaya baada ya kupigwa kwa vifaa butu na genbe la vijana wenye ghadhabu.
Afisa huyo aliyejeruhiwa alipata majeraha mabaya kwenye mkono wake wa kushoto na tumboni wakati wa makabiliano hayo kabla ya kukimbizwa hospitalini na Wasamaria Wema, akiwemo mwandishi wa taarifa hii aliyekuwa eneo la kisanga.
Bi Ngari alisema kufikia wakati wa kisa hicho, walikuwa wameharibu magunia 50 ya mchele uliolaaniwa kabla ya vijana hao wakorofi na waliokuwa wamejihami kuzima misheni hiyo na kusababisha afisa wa polisi wa kike kujeruhiwa.
Kamishna wa Kaunti ya Uasin Gishu alikashifu kisa hicho akiwashutumu wahuni kwa kuingilia shughuli hiyo.
“Tulilazimika kusitisha azma yetu ya kuharibu mchele husika baada ya kile kilichotokea. Wahusika wa shambulio hilo hivi karibuni watakabiliwa na sheria,” alisema Bw Nyale.
Leave a Reply