MAMIA ya waumini kutoka maeneo mbalimbali nchini wameshutumu utekaji nyara ambao umeongezeka na mauaji ya wale ambao wanaonekana kutofautiana na serikali ya Kenya Kwanza.
Wakiongea mnamo Ijumaa wakati wa ibada ya toba wakiangalia Mlima Kenya, waumini hao walilaani visa vinavyoendelea kuongezeka vya vijana kutekwa nyara na mauaji. Ibada hiyo ilifanyika eneo la Samson Corner, Kaunti ya Kirinyaga.
Wakitazama Mlima Kenya, waumini hao walimlilia mwenyezi Mungu ili awanusuru vijana ambao wametekwa nyara huku wakishutumu serikali kwa kuhusika na visa hivyo na kukanusha ukweli.
Walikuwa wamevalia mavazi meupe huku wakiwa wamejifunga riboni za samawati, mavazi ambayo huzingatiwa kama yaliyo takatifu wakati wa ibada.
“Tuko hapa kumwomba Mwenyezi Mungu ili atusaidie kuhimili changamoto ambazo zinakumba nchi hasa utekaji nyara. Serikali inasema haihusiki na haijui nani anawateka na kuwaua watoto wetu,
“Kama serikali haiwezi kuwahakikishia raia usalama wao, basi lazima tujilinde,” akasema Wakili Ndegwa Njiru ambaye alihudhuria maombi hayo.
Mzee Samuel Kamitha, naye alisema kuwa Kenya ipo katika mkondo ambao sheria haiheshimiwi tena. Waumini hao walitangaza vita vya kiroho dhidi ya changamoto ambazo zinakabili nchi ikiwemo utekaji nyara.
“Tunashutumu mauaji hayo na kutekwa nyara kwa vijana. Kupitia maombi tutavishinda vita hivi,” akasema Bw Karanja Mwangi, muumini.
Mzee Kamitha alisema wamekuwa wakitekeleza maombi wakizunguka Mlima Kenya mara saba kwa mwaka. Kipindi hicho wao hutoa kafara kwa Mwenyezi Mungu na kabla ya kuelekea mlimani, waumini hunyunyiziwa maji matakatifu.
Waumini hao waliotoka dini za Kiislamu, Kikristo na wale wanaobudu kwa njia za kitamaduni, walitoa ushuhuda kuwa maombi hayo yamezaa matunda miaka ya nyuma.
“Kupitia maombi hayo, wengi wamepona magonjwa na biashara za watu zimenawiri. Maombi haya pia yameleta amani nchini na hatutakoma hadi changamoto za sasa zitokomee,” akasema muumini mwingine.
Awali, waumini hao walivua viatu na kuomba kando ya vichaka huku wakimlilia Mungu akubali dua zao wakianza kuzunguka mlima. Baadhi walionekana kutokwa na maji huku wengine wakiongea kwa ndimi.
“’Kila mwaka tarehe kama hii huwa tunakongamana hapa na kumwomba Mungu atupee amani na kuwalinda watoto wetu kutoka kwa mwovu shetani,” akaongeza.
Pia waumini hao waliwaombea vijana ambao wamelemewa na uraibu wa kutumia dawa za kulevya.
Leave a Reply