Man City balaa, Man Utd goigoi: nani atawika leo?


PEP Guardiola leo Jumapili atapata usingizi mtamu ikiwa vijana wake wa Manchester City watanyamazisha Manchester United ugani Etihad baada ya kukiri matokeo duni yamemkosesha usingizi na hamu ya kula.

Kocha huyo Mhispania hakuwa ameonja ushindi mara saba mfululizo kabla ya kufyeka Nottingham Forest 3-0 hapo Desemba 4.

Ilidhaniwa kuwa mabingwa hao wa Uingereza walikuwa wamefufuka, lakini wataingia debi hiyo ya Manchester bila ushindi mara mbili mfululizo ikiwemo kuzamishwa 2-0 mara ya mwisho walikuwa uwanjani dhidi ya Juventus kwenya Klabu Bingwa Ulaya hapo Desemba 11.

Namba nne City sasa wana ushindi mmoja katika michuano 10 iliyopita msimu huu. Inamaanisha kuwa vijana wa Guardiola wataanza mechi hii na asilimia ndogo ya kuishinda licha ya kuwa wanajivunia kupepeta mashetani wekundu wa United mara nne mfululizo ligini ugani Etihad.

Man United wana motisha

United ya kocha Ruben Amorim inayokamata nafasi ya 13 itajibwaga uwanjani Etihad na motisha ya kuandikisha ushindi wa tatu mfululizo kwenye Ligi ya Uropa baada ya kulemea Viktoria Plzen 2-1 katika Jamhuri ya Czech mnamo Desemba 12.

Hata hivyo, United walisalimu amri mara mbili mfululizo ligini. Walikubali kichapo cha 2-0 kutoka kwa Arsenal (Desemba 4) na Forest 3-2 (Desemba 7) ligini.

City watakosa huduma za beki wa pembeni kulia Rico Lewis kutokana na adhabu ya kulishwa kadi mbili za njano katika sare ya 2-2 dhidi ya Crystal Palace hapo Desemba 7.

Majeraha

Kukosekana kwa Lewis kuonaongeza shida za City katika safu ya ulinzi kwani John Stones, Manuel Akanji na Nathan Ake wako mkekani. Rodri na Oscar Bobb nao wako nje kwa muda mrefu.

United hawana hofu ya majeruhi isipokuwa Luke Shaw ambaye bado ni shabiki tu kutokana na kuwa na jeraha. Jonny Evans, Victor Lindelof na Toby Collyer wamesharejea mazoezini baada ya kupona.

United walipepeta City 2-1 katika fainali ya Kombe la FA mnamo Mei 5 na pia kuwapa dozi sawa na hiyo katika Kombe la Ngao mnamo Agosti 10. Watakuwa wakifukuzia ushindi wa tatu mfululizo katika mashindano yote dhidi ya City.

Nyota Erling Haaland na Phil Foden wanaokaribia rekodi ya Sergio Aguero ya mabao manane katika gozi la Manchester, wanatarajiwa kutegemewa na Guardiola katika utafutaji wa mabao wakisaidiwa na kiungo mbunifu Kevin De Bruyne.

Nahodha wa United, Bruno Fernandes ni mmoja wa wachezaji wa kutegemewa kambini mwa United.

Imetafsiriwa na Geoffrey Anene



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*