![DNRAILAAU13121-1320x792.jpg](https://informationcentre.co.ke/wp-content/uploads/2025/02/DNRAILAAU13121-1320x792-678x381.jpg)
KIONGOZI wa Upinzani Raila Odinga Jumatatu alisema kuwa atakubali matokeo ya kura ya uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) na atarejea nyumbani iwapo azma yake haitafanikiwa.
Uchaguzi huo utafanyika mnamo Februari 15 wakati wa mkutano wa Marais wa Afrika jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Akiongea katika ukumbi wa Bomas mnamo Jumatatu, Bw Odinga alisema ameshiriki chaguzi nyingi kama mwaniaji na iwapo atabwagwa Jumamosi, atarudi nyumbani na kuendelea na shughuli zake kama kawaida.
“Kwa imani ya Mwenyezi Mungu, najua nitapata ushindi. Nikishinda tutakuwa tumeshinda na hata tukishindwa, bado tutakuwa washindi,” akasema Bw Odinga akisisitiza kuwa uchaguzi huo si suala na kifo kwake.
Alikuwa akihutubia ibada ya maombi iliyoongozwa na viongozi wa ODM na vuguvugu la wanawake katika chama hicho.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa kidini na wageni wengine ambao waliombea ushindi wa Bw Odinga kabla ya kuondoka kwake kuelekea Addis Ababa mnamo Alhamisi.
“Uchaguzi utaandaliwa Jumamosi. Nikishinda, itakuwa sawa, nikikosa, pia ni sawa. Nitarudi nyumbani na ninashukuru sana kwa maombi yenu,” akaongeza huku akisema kuwa yupo tayari kwa kazi ya kuongoza bara la Afrika.
Huku muhula wa kuhudumu kwa Moussa Faki ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa AUC ukikaribia kukamilika, Bw Odinga anategemea kupata uungwaji mkono wa Marais wa Afrika ili ashinde wadhifa huo.
![](https://informationcentre.co.ke/wp-content/uploads/2025/02/dnRaila201210.jpg)
Awali, aliwahi kusema kuwa ni viongozi wa Afrika ndio walimshajiisha awanie wadhifa huo kwa imani kuwa weledi na uzoefu wake utasaidia kushughulikia changamoto za bara hili.
“Waliniambia kuwa matatizo yanayoathiri Kenya ni sawa na yale yanayoathiri Afrika,” akasema.
Bw Odinga anaonekana kifua mbele kwenye kinyang’anyiro hicho japo anatarajiwa kupata ushindani mkali kutoka kwa Mahamoud Ali Youssouf ambaye ni Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Djibouti. Pia aliyekuwa waziri wa masuala ya nje ya Madagascar, Richard Randriamandrato, yupo debeni.
Hapa nchini, Rais William Ruto amekuwa akiongoza kwa vitendo kuonyesha uungwaji mkono kwa uwanizi wa Bw Odinga. Wiki jana, Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki akiwa jijini Kisumu alieleza imani yake kuwa Bw Odinga atawahi kiti hicho cha AUC.
Sekretariati ya kampeni ya Raila ilisema waziri huyo mkuu wa zamani amepata uungwaji mkono wa mataifa 28 japo mshindi katika raundi ya kwanza anahitajika kuwa na uungwaji mkono wa nchi 33.
Katika ngome yake ya Nyanza, Askofu wa Kanisa la Power of Jesus Around the World, Washington Ogonyo Ng’ede, amesema kuwa wiki hii ni maombi na kufunga hadi Bw Odinga afanikiwe kwenye azma yake AUC.
Viongozi wa ODM wanatarajiwa kuendeleza misururu ya mikutano ya maombi kuelekea Jumamosi wakiwa na matumaini mara hii ‘Baba’ atafanikiwa baada ya kushindwa kwenye chaguzi tano za urais.
Leave a Reply