Maraga akemea serikali kuhusu utekaji nyara – Taifa Leo


ALIYEKUWA  Jaji Mkuu David Maraga amelaani visa vya hivi majuzi vya utekaji nyara na mauaji yaliyoshuhudiwa mwaka huu akitaka Wakenya waliotekwa nyara waachiliwe mara moja.

Katika ujumbe wa mwaka mpya kwa Wakenya, Bw Maraga alikosoa vikali serikali kwa kupuuza utawala wa sheria na maadili ya utawala.

“Mwaka huu haujakuwa rahisi kwa familia nyingi. Mauaji, ulemavu na utekaji nyara wa vijana wa Kenya uliweka mtihani mkubwa katika taasisi zetu. Inahitaji jibu la kimaadili. Ikiwa sisi ni watu walioapishwa kulinda utakatifu wa maisha na hadhi ya kila raia, basi lazima tusimame kwa ujasiri katika ukweli wa Katiba yetu,” ilisema sehemu ya ujumbe wa Bw  Maraga.

“Ninalaani mauaji, mateso, na utekaji nyara na ninatoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa vijana ambao bado wanazuiliwa kinyume cha sheria. Siasa zetu zisiwe tena za kihuni na kutojali,” Maraga aliongeza.

Ujumbe wa Maraga ulijiri huku nchi ikikabiliwa na hali mbaya  mwisho wa mwaka kufuatia kuongezeka kwa visa vya utekaji nyara na kutoweka kwa watu. Utekaji nyara huo unadaiwa kusababishwa na kuongezeka kwa ukosoaji wa serikali ya Rais Ruto huku Wakenya wakitaka uongozi bora na utoaji huduma.

Hawajulikani waliko

Ripoti ya hivi majuzi ya Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu Kenya (KNCHR) ikifichua kuwa tangu Juni 2024 takriban Wakenya 82 wameripotiwa kutekwa nyara huku 29 wakiwa bado hawajulikani walipo. Haya yanajiri licha ya ahadi ya hivi majuzi ya Ruto ya kukomesha visa vya utekaji nyara nchini.

Maraga, katika taarifa hiyo, aliongeza kuwa 2024 ilishuhudia utimilifu kamili wa Katiba ya Kenya muda mrefu baada ya kuanza kutumika 2010 kupitia maandamano yaliyoongozwa na vijana Juni-Julai.

“Uaminifu kwa Katiba ni jambo la msingi. Inatuweka sisi sote i katika wajibu wetu wa kujenga jamii yenye uadilifu. Wakenya walipopigia kura kwa wingi katiba mpya mnamo Agosti 2010, waliweka maono mapya ya kubadilisha nchi na taifa,” alisema.

“Haya ndiyo maono yaliyokuwa kiini cha maandamano ya kitaifa ya Juni-Julai yaliyopewa jina la “Gen Z”. Ilikuwa nia ya Wakenya kutoka matabaka mbalimbali kuchukua jukumu la hatima yetu ya pamoja. Ilikuwa ni nia ya kushughulikia tamaduni ya kutojali na kukabiliana na uzembe na mitazamo ya kutoitikia masuala ya umma,” Maraga alibainisha.

Mwaka  ujao, Bw Maraga alitoa wito wa kuzingatiwa kwa Katiba kikamilifu, akibainisha kuwa inatoa miundo ya wazi na iliyobainishwa ya utawala, maadili na utawala wa sheria.

Huku akiitaja Katiba kuwa ahadi iliyotolewa na Wakenya, Maraga alibainisha kuwa kutii sheria za nchi kutahakikisha  maadili na kanuni za kimsingi za binadamu zitachukua nafasi ya kwanza.

maadili ya utawala

“Tunapokaribisha Mwaka Mpya, natoa wito kwetu sote kutafakari kuhusu ahadi ambayo tulijitolea miaka 14 iliyopita. Tulifafanua njia wazi ya maisha yetu ya baadaye. Tuliweka  maadili ya utawala na viwango vya ubora kama mwanga wetu wa kuongoza,” alisema.

Hata hivyo, maadili na kanuni hizi zinaweza kutimizwa pale tu zitakapokuwa  kweli kwangu na kwako wakati uadilifu na unyenyekevu ni mambo ya kwanza tunayokutana nayo kwenye milango ya ofisi zetu wakati ukweli na haki ni wino unaopita kwenye kalamu zetu kazini., utu na uwajibikaji ni nguvu zinazochochea kazi yetu,” Maraga alisema.

“Kilio cha uchungu na hasira tulizoona mwaka huu kilichochewa na mmomonyoko wa utu wa msingi na usimamizi mbovu wa kiuchumi. Ni lazima tushughulikie kwa haraka kudorora kwa sekta muhimu kama vile elimu na afya,” alieleza.

“Lazima tuweke upya uchumi ili kuunda nafasi za kazi zenye staha kwa vijana wetu na kurekebisha mfumo wetu wa ushuru ili kuhakikisha usawa na kupunguza  mzigo wa ushuru. Hili linawezekana. Nchi imefanya hivi hapo awali na inaweza kufanya tena,” Maraga alikariri.

Hata hivyo, Maraga alipongeza moyo wa Wakenya wa kutotamauka katika hali ngumu, akiangazia juhudi zao za kudai uwajibikaji kutoka kwa viongozi wao. Hata hivyo, alishikilia kuwa jukumu la jumla la utawala bora ni la wale walio madarakani.

“Mwaka huu pia umeonyesha uthabiti wa watu wa Kenya katika hali ngumu. Tumeona Wakenya wakichukua mamlaka kikamilifu na kushikilia taasisi zetu za umma kuwajibika na kuongoza njia katika kudai uwajibikaji kama ilivyoainishwa katika Katiba, hata walipokabiliana na nguvu za kikatili za serikali,” akasema.

“Nataka kuweka wazi. Jukumu la kuhakikisha kuwa vyombo vya mamlaka havitumiwi vibaya ni la viongozi,” aliongezaMaraga alitoa wito kwa serikali kuhakikisha kuwa mwaka ujao wa 2025 utakuwa mwaka wa uwajibikaji baada ya hali ngumu iliyoshuhudiwa 2024  kwa kufuata Katiba, utawala wa sheria na haki.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*