CHAI ni moja ya mazao yanayolimwa kwa wingi nchini na ina mtandao pana wa wafanyakazi.
Ikiwa inakuzwa katika mashamba makubwa eneo la Kati na Bonde la Ufa, zao hili linaiweka Kenya kwenye orodha ya wauzaji wakuu duniani.
Na kadri dunia inavyohamia katika matumizi ya teknolojia ya kidijitali, ndivyo sekta hii inavyostawi.
Teknolojia za kisasa katika kilimo hazichangii tu kuongeza kiwango cha uzalishaji, bali pia zinaongeza ufanisi na kurahisisha kazi.
Wakulima wa majanichai Githunguri, Kaunti ya Kiambu ni miongoni mwa wanaojivunia kukumbatia bunifu na teknolojia za kisasa kuboresha zaraa.
Hii ni kutokana na mashine ya kisasa, ambayo inahamasishwa na Shirika la Ustawi wa Majanichai Nchini (KTDA) kurahisisha shughuli za mavuno.
Kulingana na wakulima wa chai Githunguri, wanapitia changamoto kupata vibarua.
“Tunaopata, wanatoka nje ya eneo letu,” Samuel Njuguna, mkulima anasema.
Mtambo wa kisasa unaopigiwa upatu na KTDA, hata ingawa baadhi ya maeneo kama vile Bonde la Ufa umepokea pingamizi, kwa siku unavuna zaidi ya kilo 150.
“Unapunguza gharama ya kazi,” Njuguna anaelezea.
Catherine Wanjiku, ni mkulima mwingine anayefisia kuzinduliwa kwa mashine hiyo.
Anasema inasaidia kuokoa gharama ya mavuno, hasa kwa kuajiri vibarua bei ya chai ikiwa ingali duni.
“Wafanyakazi hulipwa Sh10 kwa kila kilo inayovunwa, bei ya sasa ya chaini ya chini mno kwani tunalipwa Sh21. Kwa sababu ya upungufu wa wafanyakazi, wakati mwingine tunapoteza mazao,” Wanjiku anaambia Taifa Dijitali.
Badala ya kutumia nguvu za umeme ikizingatiwa kuwa ni mtambo wa mikono, kawi inatumia betri ya volti 24.
Mashine hii inayouzwa Sh30, 000, betri yake inadumu kati ya saa nane hadi kumi, kulingana na matumizi.
Licha ya tija zake, mtambo huu hauna uwezo kuchuja au kutambua chai isiyotakikana – ambayo haijaafikia ubora.
“Ni teknolojia nzuri, na tunaomba iboreshwe zaidi ili kukwepa upotevu wa mazao,” anahimiza Kimani Kinyanjui.
Matumizi, mashine hii ina tahadhari ambazo mkulima anapaswa kuzingatia, ikiwemo kuvaa glovu, vidude vya maskio kuzuia kelele, miwani na gambuti.
Haipaswi kuendeshwa wakati wa msimu wa mvua.
Ukumbatiaji teknolojia za kidijitali na bunifu za kisasa, kunatajwa kuvutia vijana kwenye shughuli za kilimo na biashara.
Leave a Reply