Maswali kampuni inayosimamia e-citizen ikilipwa Sh1.45 bilioni – Taifa Leo


MASWALI yameibuka baada ya Kampuni moja ya kibinafsi inayosimamia tovuti ya e-citizen kulipwa Sh1.45 bilioni mwaka wa kifedha uliokamilika Juni 2024.

Maelezo mapya yanaonyesha kampuni hiyo ilitoa huduma mbalimbali kwa Wakenya zaidi ya mara milioni 11 na kupata Sh591.9 milioni.

Pia kampuni hiyo, Pesaflow ililipwa Sh857 milioni kwa kudhibiti na kusimamia tovuti ya e-citizen.

Haya yanakuja wakati ambapo wabunge wiki jana walishinikiza Hazina Kuu ya Fedha iweke wazi mkataba ambao kampuni hiyo ilitia saini na serikali.

“Pesa hizo zilistahili kushughulikia kudhibiti na kusimamia tovuti ya e-citizen,” akasema Mkaguzi wa Bajeti Nancy Gathungu.

Pesaflow ilichapishwa kwenye gazeti kama kampuni ambayo inastahili kukusanya pesa za e-citizen kwa niaba ya serikali wakati utawala wa Kenya Kwanza ulipoingia mamlakani.

Kampuni hiyo ilichukua kazi hiyo kutoka kwa Webmaster Kenya na Webmasters Afrika ambayo ilisimamia e-citizen kwa karibu miaka 10. Kampuni hizo zilimilikiwa na James Ayugi na ndizo zilianzisha tovuti hiyo.

Awali Webmaster iliipa kandarasi Goldrock Capital ya kukusanya mapato kwa niaba ya serikali e-citizen ilipoanzishwa lakini kampuni hizo zikatengana.

Goldrock ilielekea mahakama na kushtaki Webmasters na Hazina Kuu ya Kifedha mnam0 2016. Utawala huu ulipoingia mamlakani, pande zote zilielewana na Goldrock ikalipwa kiasi cha pesa ambacho hakikufichuliwa.

Seneta wa Busia Okiya Omtatah naye ana kesi kortini aliyoiwasilisha kupinga Pesaflow kupewa mkataba wa e-citizen.

Bi Gathungu ameibua maswali akisema tovuti ya e-citizen inaendeshwa bila msingi au njia mbadala ya kulinda data za Wakenya.

Iwapo itafeli kuendelea kutoa huduma, Bi Gathungu anasema data ya Wakenya itakuwa hatarini kuanikwa kwa kuwa kampuni hiyo ni ya kibinafsi.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*