MIILI ya vijana wawili miongoni mwa watatu waliotekwa nyara mwaka uliopita mjini Mlolongo, kaunti ya Machakos, ilipatikana Alhamisi, siku ambayo Inspekta Jenerali wa polisi Douglas Kanja na Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) Mohammed Amin walifika kortini.
Mili ya Justus Mutumwa Musyimi na Martin Mwau ilipatikana katika mochari ya jiji la Nairobi jana.Licha ya polisi kupeleka mili hiyo katika mochari ya jiji la Nairobi na kufanya uchunguzi kuitambua, Bw Kanja na Bw Amin walisisitiza mahakamani kwamba, hawakuwa na habari kuhusu vijana hao walikokuwa.
“Ninaweza kuthibitisha kwamba hakuna mmoja wa wanaume hao anazuiliwa nasi (polisi). Lakini ninataka kuhakikishia Wakenya kwamba wako salama,” Bw Kanja aliambia Jaji Chacha Mwita.
Alisema ripoti kuhusu kutekwa nyara kwa watatu Justus Mutumwa, Martin Mwau na Karani Muema iliwasilishwa katika kituo cha polisi cha Athi River na DCI ikaanza uchunguzi kwa kufuatilia simu zao.
Bw Amin alisema watatu hao hawakuwa wakizuiliwa na maafisa wa DCI na kwamba, uchunguzi ulikuwa ukiendelea.
“Ningetaka kusema kwamba watu hao waliopotea hawajazuiliwa na Huduma ya Kitaifa ya Polisi. Hatukuwakamata na hatuwazuilii,” Bw Amin alisema.
Bw Amin aliambia mahakama kuwa, hawakuwakamata na kuwazuilia, hawangeweza kutoa mili yao au kuwafikisha kortini kuwafungulia mashtaka yoyote.
Hata hivyo, Daniel Maanzo, wakili wa Bw Mutumwa alisema kwamba familia ya mwanamume huyo ilipata mwili wake katika mochari ulikopelekwa na polisi baada ya kupatikana eneo la Ruai kaunti ya Nairobi.
Wakili Dan Maanzo alisema kauli za polisi mbele ya mahakama zinaashiria kwamba walidanganya, idara na vitengo vya usalama havifanyi kazi kwa kushirikiana au Wakenya hawako salama chini ya polisi.
Leave a Reply