RAIS William Ruto aliacha wakazi wa Machakos na maswali mengi kwa kuepuka siasa alipozuru ngome ya kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka mnamo Ijumaa.
Kiongozi wa nchi alikuwa katika Kaunti za Machakos na Makueni kwa mahafali ya 59 ya Chuo Kikuu cha Scott Christian na kuzindua kituo cha Timbuktoo katika eneo la Konza Technopolis.
Tofauti na maeneo mengine anayozuru ambako anazungumzia siasa baada ya hafla rasmi, Rais Ruto aliondoka katika hafla hiyo na kufululiza moja kwa moja hadi Konza bila kukutana na wakazi.Wabunge wa chama cha UDA, Vincent Musyoka (Mwala) na Nimrod Mbai (Kitui Mashariki) walikosekana katika msafara huo na kuzua uvumi kwamba mambo hayakuwa sawa kati ya Rais na washirika wake Ukambani.
Jambo la kushangaza ni kwamba wabunge Caleb Mule (Machakos Mjini), Joshua Mwalyo (Kibwezi Mashariki) na Mwengi Mutuse (Kibwezi Magharibi), walioandamana na Rais Ruto hadi Chuo Kikuu cha Scott Christian hawakuruhusiwa kuzungumza.
Gavana wa Machakos na viongozi wengine wa Wiper katika kaunti hiyo walisusia hafla ya Rais Ruto. Katika Kaunti ya Makueni, Gavana wa Makueni Mutula Kilonzo Jr na Mbunge wa Kilome Thaddeus Nzambia walimsifu Rais Ruto kwa ujenzi wa jiji la Konza Technopolis na bwawa la Thwake katika mpaka wa Kitui na Kaunti ya Makueni.
Ziara hizo zilijiri wakati eneo la Ukambani linachangamkia ushirikiano uliopendekezwa na Mlima Kenya baada ya Chama cha Gikuyu, Embu na Meru kujumuisha jamii ya Akamba.
Ziara hiyo pia ilijiri wakati ambao manung’uniko makali kati ya washirika wa Rais Ruto katika eneo hilo yanatanda. Kwa sauti za chinichini, wanasema kuwa kiongozi wa nchi ametenga eneo hilo katika masuala ya maendeleo na uteuzi serikalini.
Aliyekuwa Mbunge wa Machakos Mjini Victor Munyaka, ambaye zamani alikuwa mshirika wa Rais Ruto, amekuwa akimkosoa Rais kwa anachodai utawala mbaya. Hili limemfanya achangamkiwe na washirika wa Bw Musyoka ambao wamekuwa wakiwapatia washirika wa Rais Ruto Ukambani wakati mgumu.
Bi Ndeti, Seneta wa Machakos Agnes Kavindu na mwenzake wa Makueni Daniel Maanzo walitoa wito kwa eneo hilo kuwakataa washirika wa Rais Ruto.
Leave a Reply