UAMUZI wa jamii ya Gusii kumuunga waziri wa zamani wa Usalama Fred Matiang’i kisiasa utavuruga hesabu za vyama vya Orange Democratic Movement (ODM) na United Democratic Alliance (UDA) kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Mnamo Jumanne wiki hii, Seneta wa Kisii Richard Onyonka alitangaza kuwa jamii hiyo itaunga azma ya urais ya aliyekuwa Waziri wa Usalama Fred Matiang’i katika uchaguzi huo chini ya mwavuli wa chama kimoja cha kisiasa bali sio ODM au UDA.
“Tunapanga kuwa na chama chetu cha kisiasa ambacho kitaendeleza masilahi yetu katika ngazi ya kitaifa,” Bw Onyonka akasema kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.
“Kwa hivyo, tumeamua kuwa tutamuunga Dkt Fred Matiang’i kama mgombeaji wetu wa urais katika uchaguzi mkuu ujao. Atawania urais kwa tiketi ya chama ambacho kitasukwa kwenye msingi wa haki, uwazi na maadili, ajenda yake kuu ikiwa ni utoaji huduma,” Seneta huyo wa Kisii akaongeza.
Kulingana na Seneta Onyonka, lengo lao ni kuhakikisha kuwa wanasiasa wote, pasi na kujali miegemeo yao ya kisiasa, wanaunga mkono ndoto ya Dkt Matiang’i.
Tangazo la Bw Onyonka lilijiri siku chache baada ya Dkt Matiang’i kukutana na wabunge 10 kutoka kaunti za Kisii na Nyamira kama sehemu ya mikakati yake ya kusaka uungwaji kutoka eneo hilo anakotoka kabla ya kupanua mawanda yake maeneo mengine ya nchi.
Isitoshe, azma ya urais ya Dkt Matiang’i inaonekana kupata nguvu baada ya duru kusema kuwa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta yuko nyuma yake.
Ni kwa misingi hii ambapo swali limeibuka kuhusu iwapo Dkt Matiang’i atafaulu katika safari ya Ikulu iliyomlemea aliyekuwa kigogo wa siasa za jamii ya Gusii marehemu Simon Nyachae mnamo 2002.
Bw Nyachae aliwania urais mwaka huo, kwa tiketi ya chama cha Ford People, na kumaliza wa tatu kupata kura 345,152 pekee katika kinyang’anyiro ambacho Marehemu Mwai Kibaki alishinda kwa kupata kura 3,546, 277.
Kwenye mahojiano na safu hii, Bw Onyonka alikwepa swali hilo huku akishikilia “haja yetu kuu ni kuwa na usemi katika ngazi ya kitaifa.”
“Hilo la iwapo Matiang’i atashinda au la tuachie Mungu. Ilivyo sasa sisi kama jamii ya Ekegusi hatujapata haki haswa katika ugavi wa nyadhifa za uongozi katika ngazi ya kitaifa. Tunaamini kuwa kuungana kwetu kutatusaidia kupata haki yetu katika ngazi ya kitaifa,” akaeleza.
Kulingana na takwimu kutoka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kaunti za Kisii na Nyamira zilikuwa na jumla ya wapiga kura 960,293 kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.
Hata hivyo, maelfu ya watu kutoka jamii ya Gusii ni wapiga katika miji mingine mikubwa nchini, likiwemo jiji la Nairobi.
Hii ina maana kuwa ili aweze kuwa tishio kwa wagombeaji wakuu kama Rais William Ruto, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Dkt Matiang’i atalamika kusaka uungwaji mkono mkubwa kutoka maeneo mengine ya nchi.
Mbunge mmoja kutoka kaunti ya Kisii ameambia safu hii kwamba chama kinachoandaliwa kuwa “chama cha jamii ya Ekegusi” ni United Progressive Alliance (UPA).
Inaaminika kuwa “mmiliki halisi” wa chama hicho kinachoongozwa na Gavana wa Nyamira Amos Nyaribo ni Dkt Matiang’i.
Akiongea baada ya kuongoza mkutano wa Baraza la Kitaifa la Uongozi (NGC) mjini Nyamira hivi majuzi, Bw Nyaribo alieleza kuwa iliamuliwa baadhi ya nyadhifa za uongozi katika chama hicho ziachiwe watu kutoka maeneo mengine ya nchi.
“Hii ni sehemu ya mikakati yetu ya kukipa chama hicho sura ya kitaifa kando na kukipa nguvu zaidi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027,” akaeleza, akiashiria kibarua cha kitaifa cha Dkt Matiang’i.
Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Dismus Mokua anasema vyama vya ODM na UDA vitapoteza zaidi endapo Dkt Matiang’i atawania urais kwa tiketi ya UPA.
“Siasa za Kenya huwa ni za kikabila, kwa hivyo, bila shaka azma ya Dkt Matiang’i itapata uungwaji mkubwa kutoka eneo la Gusii. Na hata akifeli chama chake kitashinda idadi kubwa ya viti, hali itayokampa nguvu ya kufanya mazungumzo na mshindi wa urais kwa nia ya kufanya kazi pamoja. Hali kama hiyo ilifanyika Afrika Kusini mwaka jana,” anaeleza.
Leave a Reply