Mazingira ambapo [ni] hutumiwa kutoa amri – Taifa Leo


TULITAMATISHA sehemu ya kwanza ya msururu huu kwa kutaja kwamba kiambishi {ni} katika neno ‘tokeni’ kinatekeleza kazi ya wingi katika nafsi ya pili.

Ikumbukwe kuwa ni katika nafsi hiyo tu ambapo msemaji hashurutiki kutaja kiwakilishi cha nafsi kiambata.

Akihiari kutumia kiwakilishi hicho, basi kiambishi {ni} huwa hakijitokezi tena kwenye kitenzi husika. Nilivyoeleza katika sehemu ya kwanza ya makala, haiyumkiniki kusema ‘mtokeni!’ ila tunasema ‘mtoke!’

Baadhi ya wanasarufi wanaeleza kuwa viwakilishi nafsi huwakilisha (nimerudia neno ‘wakilisha’ kwa kutokuwa na neno jingine mwafaka la kutumia katika muktadha huu) viumbe wenye uhai tu.

Ninatofautiana na maoni haya kwa sababu ni jumlishi mno! Waama, si viumbe wote wenye uhai ambao wana uwezo wa kujirejelea na kuwarejelea wengine isipokuwa binadamu tu.

Kwa njia nyingine na katika hali halisi, ni binadamu tu anayeweza kusema ‘mimi’ na ‘wewe’.

Inasadifu tu kuwa kiwakilishi cha nafsi ya tatu; umoja na wingi kinaweza kutumiwa kurejelea binadamu na viumbe wengine wenye uhai.

Mathalani, inayumkinika kutoa kauli kama hii: Wao ni wanyama wanaopenda kuwinda wakiwa kwenye makundi.

Inasadifu pia kuwa viwakilishi vya nafsi viambata katika nafsi ya tatu yaani {a} na {wa} ni kitambulisho muhimu cha ngeli ya A-WA ambayo inajumuisha viumbe wote wenye uhai.

Alhasili, katika neno ‘tokeni!’ kiambishi {ni} ni cha wingi bali si cha kutoa amri. Hata hivyo, alama ya hisi ndiyo inayothibitisha kuwepo kwa amri yenyewe hasa katika lugha andishi.

…MAKALA YATAENDELEA
[email protected]



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*