MPANGO wa mazishi ya mmoja wa watu waliofariki baada ya kuangukiwa na ukuta katika eneo la Miritini, Kaunti ya Mombasa, ulitibuliwa dakika za mwisho baada ya familia kuambiwa lazima mwili ufanyiwe upasuaji kubainisha chanzo cha kifo.
Hayo yalijiri huku ikibainika idadi ya waliofariki ilifika sita.
Mwili wa Abdallah Timothy, 24, uliokuwa umeandaliwa kwa mazishi ya Kiislamu, ulikuwa tayari kupelekwa msikitini kwa sala ya mwisho wakati polisi walifika na kusitisha shughuli hiyo.
“Wamechukua mwili, tumelazimika kuahirisha mazishi. Polisi wamesema lazima uchunguzi wa maiti ufanywe kabla ya mwili kukabidhiwa familia kwa mazishi,” alisema Abu Nassoro, mjomba wa marehemu.
Waathiriwa walikuwa wakihudhuria mazishi eneo hilo Jumatatu mchana na walikuwa wamepanga foleni kutazama mwili wa jirani yao wakati maafa hayo yalipotokea.
Ukuta ulianguka kufuatia mvua kubwa iliyoandamana na upepo mkali.
Timothy alifariki katika hospitali ya Port Reitz alipokuwa amepelekwa kwa matibabu. Waathiriwa walijumuisha pia mwanamke mjamzito.
Leave a Reply