KATIKA kipindi cha miezi mitatu, afisa mkuu wa polisi amekamatwa mara mbili kwa madai ya kujituma kuhudumu kuongoza trafiki jijini Nairobi, zaidi ya kilomita 170 kutoka kituo chake cha kazi.
Naibu Afisa Mkuu wa Kituo (OCS) katika Kituo cha Polisi cha Mavindini, kaunti ya Makueni, Guyo Dida amekamatwa mara mbili baada ya kupatikana akiongoza magari ndani ya kaunti ya Nairobi.
Kituo cha polisi cha Mavindini kiko katika Kaunti ya Makueni.
Siku ya Jumanne, Bw Dida alikamatwa katika eneo la Globe Cinema Roundabout kufuatia malalamishi ya mtu aliyemwona afisa huyo akizozana na dereva wa gari, Najma Ali Magongo.
Afisa wa polisi aliyefahamu kisa hicho alisema kuwa Bi Magongo alikuwa akiendesha gari lake aliposimamishwa na afisa huyo ambaye alikuwa amevalia sare kamili.
Afisa huyo alidai kuwa alikuwa akivunja sheria za trafiki na kumtaka aendeshe gari hilo hadi kituo cha polisi.
Hata hivyo, wakiwa njiani, alidaiwa kumtaka amlipe Sh15,000 ili aachiliwe.
“Kwa bahati nzuri, msamaria mwema alishuku na akamjulisha afisa wa zamu Kituo Kikuu cha Polisi, Ambrose Kivuva. Alilizuia gari hilo katika barabara ya Slip Road,” polisi walisema.
Taarifa za mashahidi zinasema kuwa Bw Dida alikasirishwa na mwenzake aliyesimamisha gari. Bw Dida alidai afisa huyo mwingine wa polisi alikuwa akiingilia kazi yake.
Bw Dida alidaiwa kumpiga mwenzake kofi, na kusababisha ugomvi ulioishia kwa sare yake kuchanika kiasi.
Wananchi waliingilia kati, na Bw Dida alikamatwa na kuzuiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi.
Mnamo Oktoba 23, 2024, akiwa likizoni, Bw Dida alikamatwa baada ya kupatikana akiendesha majukumu ya polisi wa trafiki bila kibali katika eneo la Bunyala Roundabout katika Kaunti Ndogo ya Makadara.
Kulingana na ripoti ya polisi, maafisa kutoka Kituo cha Polisi cha Eneo la Viwandani walimkamata akiwa amevalia sare.
Pia alipatikana na kifaa cha mawasiliano mali ya Kitengo cha Polisi cha kuhudumua Watalii.
Bw Dida baadaye alikabidhiwa kamanda wa polisi wa Kaunti Ndogo ya Kathonzweni na kuzuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Makueni ili achukuliwe hatua za kinidhamu.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA
Leave a Reply