Ndugu zangu albabu, muyajuwao maisha,
Kwa wake utaratibu, wenye sifa zakuchosha,
N’zipi zenu hisabu, khabari mkatupasha,
Ai! Mbati za maisha!
Maisha yana dharubu, hukondesha nakufisha,
Hupati bila sulubu, ukipata kakitosha,
Lazima upate tabu, ndivyo yalivyo maisha,
Ai! Mbati za maisha!
Maisha yana adhabu, kwingi kutudhalilisha,
Yana na nyingi adhabu, na kwingi kutuchokesha,
Nakututia aibu, waja kutufedhehesha,
Ai! Mbati za maisha!
Maisha hutuharibu, wengine wetu kutisha,
Tukazikana nasabu, kwetu tukajihamisha,
Kwenda kuishi ghaibu, viumbe kuhangaisha,
Ai! Mbati za maisha?
Farida na zainabu, nje wakajizungusha,
Haya nyusoni meghibu, utu wameupomosha,
Muhindi kwa muarabu, na wetu kina mwanasha,
Ai! Mbati za maisha!
Maisha hutughilibu, ghafula hutuzeesha,
Kijana akawa babu, mwiliwe kuunyausha,
Akabaki masharubu, uzuri wote ukesha,
Ai! Mbati za maisha!
Mtu akawa kidhabu, haramu kuhalalisha,
Bora cha leo kuswibu, hata kikiwa chatusha,
Asikumbuke hisabu, siku hiyo yakutisha,
Ai! Mbati za maisha!
Twaishi hatuna jibu, miili ingatuwasha,
Wengi wetu ni mabubu, maisha metusozesha,
Hayatimu matilabu, kwingi kujitairisha,
Ai! Mbati za maisha!
Kila siku masaibu, hutufanya tukakesha,
Umgonjwa kujitibu, huna pesa zin’kwisha,
Uvumilie adhabu, tumbo likikuharisha,
Ai! Mbati za maisha!
N’na mengi as’habu, yakusema hayajesha,
Kuyapanga babu babu, bure n’tawachokesha,
Yatosha n’lohasibu, jambo hili kuwapasha,
Ai! Mbati za maisha!
UST. MUHAMMAD ABDALLAH (CHETEZO)
“MKINAMLUNDE”
MWANATI WA AFRIKA MASHARIKI.
MALINDI
Odinga usife moyo
Siyekubali kushindwa, hakika si mshindani,
Hata ingawa ‘metendwa, zidi kuvumilieni,
Wema wako waundwa, katika siku usoni,
Odinga usife moyo, itakuja siku njema.
Afrika ‘mezunguka, si baharini si bara,
Rwanda Togo ukafika, hadi nchi kavu sahara,
Usije ‘kababaika, sisi hatutakugura,
Odinga usife moyo, itakuja siku njema.
Taifa lakungojea, ‘shikilie upinzani,
Weye twakutegemea, kufichua yalo ndani,
Ukinzani mezembea, mithili hewa angani,
Odinga usife moyo, itakuja siku njema.
Usipandwe na hamaki, maana umepoteza,
Mahmoud ni rafiki, tuzidi kumpongeza,
Tuondoe yetu chuki, Kenya tupate aviza,
Odinga usife moyo, itakuja siku njema.
Kalamu yakwamakwama, nomba ijaza nondoke,
Raila ‘simame wima, taifa lisikucheke,
Mola akupe uzima, uishi hadi uchoke,
Odinga usife moyo, itakuja siku njema.
SHEM NYANG’ECHI ABUGA
PROF-MKEREKETWA,
NAIVASHA
Kupenda upuzi
Ukurasa nafungua, kuyasema ya moyoni,
Nafsi imeugua, kuniletea huzuni,
Wallahi nimegundua,leo nakula yamini,
Kupenda upuzi tupu, siku hizi nimejua.
Kupenda upuzi tupu, siku hizi nimejua,
mapenzi ni kama bupu, unata bila kujua,
Kupendwa ni kama jipu, na hisia huchujua,
Mimi sasa sitopenda, nayawachia wazungu.
Mimi sasa sitopenda, nimewachia wazungu,
Kidosho nilompenda, kamweka moyoni mwangu,
Na mwishowe kanitenda, kuua nafsi yangu,
Na kamwe sitosahau, nilivyojipata kwake.
Na kamwe sitosahau, nilivyojipata kwake,
Kapenda kama dharau, akanitoa upweke,
Mapenzi yake ni dau, lazama kwenye uvuke,
Mapenzi kanifundisha, na leo ananikana.
Mapenzi kanifundisha, leo hapa anikana,
Mwanzo kanipa bashasha, siku tulipopatana,
Huba kanichangamsha, walahi kawa dafina,
Lakini leo nasema, nimependa ukapera.
Lakini leo nasema, nimependa ukapera,
Na tupatane kiyama, Asha uliyenikera,
Uliyenipa dhuluma, nakuambia hongera,
Ukurasa naufunga, kuyasema ya moyoni.
EZEKIEL NZEKE JAMES (KARMA)
MIKOBA YA BABU
MBUINZAU
Penzi la ovadozi
Kwa myaka niliugua, nusu miye kujifia,
Waganga wakagangua, patupu kuambulia,
Maradhi yalosumbua, upofu yakanitia,
Penzi lako ovadozi, tiba imeniingia.
Tangu nyonda kukujua, maradhi sijayapata,
Twiba umeigundua, sijui kama limbwata,
Huba lako napumua, mishipa moyo yanata,
Penzi lako ovadozi, tiba imeniingia.
Mwenzi umenizuzua, majununi nimebaki,
Unanipa vya halua, mbali nawe sibanduki,
Huba ninasukutua, wasugua ja mswaki,
Penzi lako ovadozi, tiba imeniingia.
Tena ukinikagua, nabaki kuchekacheka,
Macho sikio na pua, na shingoni ukishuka,
Ukifika kwa kifua, hoi najitepwereka,
Penzi lako ovadozi, tiba imeniingia.
Wewe nimekuchagua, duniani na ahera,
Hani kwako ninatua, kwingine sina papara,
Mwili nimetutumua, hani nitoe kafara,
Penzi lako ovadozi, tiba imeniingia.
Waridi umechanua, uturi wanimaliza,
Moyo umeuchukua, mapigo kwako yacheza,
Chunga usijeniua, famili ukawaliza,
Penzi lako ovadozi, tiba imeniingia.
Joto likinitibua, daktari walishusha,
Baridi ikizimua, dozi yako yanitosha,
Na chekapu wazijua, sina nguvu za kubisha,
Penzi lako ovadozi, tiba imeniingia.
MIRUMBE P NICKSON
“USTADHI BABU KIJANA”
Chozi la muuza sanda
Pulikani wasikizi, sikia yangu kauli,
Si ya kesi maamuzi, ndipo niliseme hili,
Bali ni kwa uchambuzi, naufichua ukweli,
Matangani si la kweli, chozi la muuza sanda!
Chozi la muuza sanda, litakuwaje la kweli,
Na iwapo hajapenda, kuuza apate mali,
Kama basi hakupenda, vije hauzi bakuli,
Matangani si la kweli, chozi la muuza sanda!
Ni kilio cha furaha, mteja kapatikana,
Mteja hawi karaha, karaha kukosekana,
Mauzo kunoga raha, sivyo nikudanganyana,
Matangani si la kweli, chozi la muuza sanda!
Hivi muuza maziwa, anapopata mteja,
Itakuwaje ni sawa, wa sanda iwe kiroja,
Achekapo wa maziwa, mwenzi chozi labubuja,
Matangani si la kweli, chozi la muuza sanda!
Ni yale ya kisebusebu, hali kijoyo ki papo,
Bahati huwa kasibu, na iletayo malipo,
Kulia huna sababu, je, wauza sanda mpo?
Matangani si la kweli, chozi la muuza sanda!
Ni wachache wanojua, chozi la mtu nafiki,
Ni kicheko laangua, kwamba kazoa riziki,
Kinywache angapanua, kifo humpiga jeki,
Matangani si la kweli, chozi la muuza sanda!
Kwenye yake karakana, seremala majeneza,
Kuunda anang’ang’ana, lengo kuu kuyauza,
Kufa hutamani sana, kwa muwele wa kulaza,
Matangani si la kweli, chozi la muuza sanda!
Yasitutie vimbimbi, machozi ya seremala,
Kwa ndani analo ombi, mtu afe si kulala,
Hivyo tuache vitimbi, halali katu si hila,
Matangani si la kweli, chozi la muuza sanda!
NYAGEMI NYAMWARO MABUKAH
“MALENGA WA MIGOMBANI”
MIGOMBA YA ZIWA KUU.
Leave a Reply