Mbunge apata pigo, ardhi aliyodai umiliki wake kutumiwa kwa ujenzi wa soko – Taifa Leo


MBUNGE wa Kiambu Town Machua Waithaka amepata pigo baada ya serikali kutenga Sh350 milioni kwa ujenzi wa soko la kisasa katika eneo la South B, eneo bunge la Starehe, Nairobi.

Soko hilo litajengwa kwenye ardhi iliyosajili LR.NO209/12612, ambayo ilizua mzozo kati ya wakazi na mbunge huyo, ambaye alidai umiliki wake.

Taifa Leo ilithibitisha barau iliyotumwa kwa Serikali ya Kaunti ya Nairobi kutoka kwa Wizara ya Ardhi Januari 9, 2025. Ilisema tayari zabuni imetolewa na kwamba sherehe ya kuweka msingi wa ujenzi wa soko hilo inatarajiwa kufanyika katika kipindi cha wiki chache zijazo.

“Hii ni kuwajulisha kuwa kazi za ujenzi wa soko la kisasa la South B zimetolewa kwa kampuni ya ujenzi ya M/s Jyan, na mkataba wa kipindi cha miezi 12. Kwa sababu hii, mnashauriwa kuwajulisha wafanyabiashara waliopo kwenye eneo husika waondoke, kwani mwanakandarasi anatarajiwa kuchukua eneo hilo kwa kipindi chote cha ujenzi,” ilisema barua hiyo.

Jumanne wiki iliyopita, wakati wa kongamano la umma, Mwakilishi wa wadi ya South B Waithera Chege, aliongoza mamia ya wafanyabiashara kusherehekea tangazo hilo.

Bi Chege alidai kuwa viongozi kadhaa wenye ushawishi walihusika katika njama ya kunyakua ardhi hiyo yenye utata. Alishukuru utawala wa Rais Ruto kuzima juhudi hizo.

Miezi kadhaa iliyopita, mahakama ilikataa kusikiliza kesi ya mbunge huyo, kufuatia ripoti zinazokinzana kuhusu thamani ya ardhi hiyo. Alidai ardhi hiyo ilikuwa ya Sh20 milioni, huku utathmini kutoka kwa serikali ikiweka thamani ya ardhi hiyo kuwa juu zaidi ya kiasi kilichotajwa.

 Soko hilo la kisasa, litakuwa la kwanza kujengwa katika Kaunti ya Nairobi kati ya masoko 20 yaliyoahidiwa na Rais William Ruto wakati wa kampeni za uchaguzi. Litatumiwa na wafanyabiashara 2,500 na kubuni ajira kwa vijana.

Ripoti ya uchunguzi iliyowasilishwa na Kamati ya Mipango Mijini chini ya mwenyekiti Alvin Olando Palapala, ilionyesha nyaraka zilikuwa zimeghushiwa ili kudai umiliki wa ardhi hiyo. Kamati  ilipendekezwa kwamba ardhi hiyo irejeshwe kutoka kwa mbunge huyo.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*