UZIBAJI gapu ya uhaba wa chakula ni mojawapo ya ajenda kuu ambayo serikali ya sasa inajikakamua kuangazia.
Kupitia mpango wa ruzuku ya mbolea, Serikali ya Kenya Kwanza inasisitiza kuwa inalenga kuhakikisha mazao yanaongezeka mara dufu.
Katika Kaunti ya Kakamega, Pasta Jacob Omolo kando na kulisha wafuasi wake chakula cha kiroho, anajituma kuona hawalali njaa.
Omolo ambaye aliingilia shughuli za kilimo 1989, amekumbatia mfumo unaojulikana kama ‘relay’ kwa Kiingereza kuhakikisha kwamba shamba lake lina mseto wa mazao.
Anafanya zaraa katika Kijiji cha Eshibimbi, Kaunti Ndogo ya Butere.
“Relay, tukitumia tafsiri yake katika riadha ni mbio za kasi kupokezana vijiti. Hivyo, katika kilimo ni mfumo wa mmea mmoja kukaribisha mwingine kwa kuupokeza jukwaa,” Pasta Omolo anasema.
Kwenye shamba lake lenye ukubwa wa ekari tatu na nusu, japo ekari mbili ndizo anatumia kukuza mimea, amelipamba kwa mseto wa mboga.
Hulima mboga za kienyeji kama vile managu, terere, kunde, sagaa, na pia sukuma wiki na spinachi.
Omolo, vilevile, hukuza mahindi na mseto wa maharagwe, viazi vikuu kama vile mihogo na nduma.
“Ninafanya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na nyuki kwa minajili ya asali,” anaelezea.
Kilimo cha relay, ni mbinu ya kukuza mazao mengi kwa mfululizo ambapo baadhi ya mazao yanashirikiana katika mizunguko ya ukuaji.
Zao la pili hupandwa kando na zao la kwanza, kabla ya kuvunwa.
Kwa mfano, eneo ambalo amepanda mboga, zinapokaribia kuisha hupanda maharagwe na mahindi.
“Mfumo huu unafanikishwa kupitia teknolojia ya kuinua undongo kwa kipimo – sawa na muundo wa vitanda,” Omolo anaelezea.
Ni mfumo maalum alioujua kupitia SNV Netherlands Development Organisation, chini ya mradi wake wa Regenerative Agricultural practices for improved Livelihoods and Markets (REALMS), uliozinduliwa 2020 na kukamilika Oktoba mwaka uliopita, 2024.
SNV ni shirika la kimataifa lisilo la kiserikali (NGO), ambalo madhumuni yake ni kukabiliana na kero ya umaskini kupitia kilimo, na linaendeleza programu kadhaa za zaraa nchini Kenya.
Programu hizo zinapania kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mfumo wa relay unajiri na faida nyingi, zikiwemo; udhibiti wa wadudu na magonjwa, kuboresha rutuba ya udongo na mzunguko wa virutubisho, na vilevile kuongeza kiwango cha mazao.
Kulingana na Omolo, kwa mkulima mwenye shamba dogo inakuwa rahisi kukuza mseto wa mimea – hivyo kuhakikisha ardhi inatumika ipasavyo.
“Kwa sababu ya udongo kuinuliwa na kupandwa mimea yenye nguvu kama vile mahindi na nyasi za mabingobingo (Napier grass), kero ya mmomonyoko inazimwa,” Mhubiri Omolo akaambia Akilimali wakati wa mahojiano shambani mwake Eshibimbi, Kakamega.
Hata hivyo, kilimo cha relay kinaweza kuwa kigumu kutekelezwa kwenye mashamba makubwa kutokana na changamoto za kudhibiti magugu na kutumia mashine za kilimo.
Katika shamba la Omolo, pia hulima mti maalum aina ya Senegalia pennata.
“Una maua yanayovutia nyuki, na majani yake huyatumia kuunda mboleaasilia,” akaelezea.
Aidha, hutengeneza mbolea inayojulikana kama bokashi – inayoundwa kwa kutumia majani ya Senegalia pennata, na ya mimea na matawi mengine, kinyesi cha mifugo, kisha inahifadhiwa kwa njia ya kipekee ili kuchacha.
Ni mbolea inayosaidia kuboresha rutuba shambani.
Wanunuzi wa mazao ya Pasta Omolo, ni wenyeji wa Eshibimbi na washirika anaolisha chakula cha kiroho.
Leave a Reply