MUHUDUMU katika sekta ya Utalii ameshtakiwa kwa kumlaghai na kumlipisha bei ghali mtalii kutoka Ubelgiji.
Patrick Kiilu Muthini aliyefikishwa kortini Januari 2, 2025 alikana kumlaghai Filip Martiens Dola za Marekani (USD-$)8,180 (KSh1,055,220).
Bw Muthini, mahakama ilielezwa, alikuwa amemhadaa Mbelgiji huyu atampeleka kuona maeneo ya ajabu nchini pamoja na kumpeleka katika hifadhi tajika za Wanyama porini kufurahia madhari ya kupendeza na kufurahisha moyo.
Hata hivyo, hakimu mkazi Rose Ndombi alifahamishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga kupitia wakili wa Serikali Ishmael Kiragu kwamba mshtakiwa alimhadaa Martiens na “hakumpeleka kule alimuahidi.”
Baadhi ya mahala ambapo Martiens angelipelekwa ni vivutio vya watalii sawia na kutembezwa hifadhi tajika za wanyama wa pori pamoja na maeneo muhimu zaidi humu nchini.
Kiongozi wa mashtaka Bw Ishmael Kiragu alieleza mahakama mshtakiwa hakutimiza ahadi yake ndipo akatiwa mbaroni.
Muhudumu huyo katika kampuni ya Safari Herd alikabiliwa na shtaka la kupokea pesa kwa njia ya udanganyifu.
Baada ya kukana shtaka hilo, mshtakiwa aliomba apewe fursa ya kusuluhisha suala hilo na chama cha watalii nchini-KATO.
“Naomba niachiliwe kwa dhamana isiyo ya kiwango cha juu ndipo nisuluhishe suala hili na mlalamishi na KATO,” mshtakiwa aliirai mahakama kupitia kwa wakili aliyemwakilisha.
Kiongozi wa mashtaka Bw Kiragu hakupinga ombi la mshtakiwa la kuachiliwa kwa dhamana ila alimsihi hakimu azingatie kiwango cha pesa alichotapeliwa mtalii huyo.
Mahakama ilimwachilia mshtakiwa kwa dhamana ya Sh500,000 ama pesa tasilimu Sh100,000.
Mahakama ilifahamishwa mshtakiwa alipokea pesa hizo kutoka kwa Martiens katika eneo la Westlands Nairobi kati ya Oktoba 4 na Desemba 30, 2024.
Kesi hiyo itatajwa baada ya wiki mbili kutengewa siku ya kusikizwa.
Leave a Reply