Miili 18 yatolewa mtoni baada ya ndege mbili kugongana angani Washington DC – Taifa Leo


WASHINGTON, AMERIKA

MIILI 18 ilitolewa mapema Alhamisi, Januari 30, 2025 kwenye Mto Potomac, Amerika kufuatia ajali ya ndege karibu na uwanja wa kitaifa wa Reagan, Washington DC.

Juhudi za uokoaji na uopoaji bado zinaendelea kutokana na ajali hiyo iliyofanyika Alhamisi asubuhi. Ndege ya abiria ilipogongana na ile ya jeshi na kushtua Amerika.

Shirika la Ndege la Amerika ambalo ndege ya abiria lipo chini yake, jana lilisema kuwa abiria 69 na rubani wanne walikuwa kwenye ndege hiyo. Wanajeshi watatu kutoka jeshi la Amerika pia walikuwa lakini hatima yao bado haijulikani.

Jana idara ya uokoaji iliweka nambari ambayo wanafamilia wa waliokuwa katika ndege hiyo wanaweza kupiga simu kuwasiliana nao kufahamu hatima ya wapendwa wao.

Rais wa Amerika Donald Trump kupitia taarifa jana alisema alikuwa amefahamishwa kwa kina kuhusu ajali hiyo na kuwa alikuwa akitathmini hali kabla ya kutoa maelezo zaidi.

“Ndege hiyo ilikuwa kwenye laini yake ikikaribia uwanja wa ndege. Helikopta ilikuwa pia ikielekea kwenye njia sawa na wakati huo mwangaza wote ulikuwa sawa uwanjani na kwenye ndege,” akasema Rais Trump.

“Mbona helikopta haikupaa au hata kugeuka kuzuia mgongano huo. Mbona idara husika ya kudhibiti idara ya uchukuzi wa angani haikuambia helikopta kile cha kufanya?,” akauliza Rais Trump akisema ajali hiyo ingeepukwa.

Hata hivyo, Rais aliwashukuru asasi mbalimbali za uokoaji ambazo zilijitokeza na akasema kuwa bado anafuatilia hali kabla ya kutoa taarifa zaidi.

Waziri wa Ulinzi Peter Hegseth naye kwenye mtandao wa X wizara ilikuwa ikifuatilia hali na ilikuwa tayari kutoa msaada wowote ambao utahitajika.

Shirika la uchukuzi wa Ndege Amerika lilisema ndege ilikuwa ikielekea Kansas kutoa Wichita kabla ya kugongana na helikopta ya jeshi.

Shughuli za ndege kutua na kuondoka kutoka uwanja wa Reagan zilisitishwa kutokana na ajali hiyo.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*